2 Nyakati 13 - Kiswahili Contemporary Scriptures 2024

Abiya mfalme wa Yuda(1 Wafalme 15:1-8)

1Katika mwaka wa kumi na nane wa utawala wa Yeroboamu, Abiya akawa mfalme wa Yuda,

2naye akatawala huko Yerusalemu miaka mitatu. Mama yake aliitwa Maaka, binti Urieli wa Gibea.

Basi kulikuwa na vita kati ya Abiya na Yeroboamu.

3Abiya aliingia vitani na jeshi la watu elfu mia nne wenye uwezo wa kupigana, naye Yeroboamu akapanga jeshi dhidi ya Abiya akiwa na jeshi la watu elfu mia nane wenye uwezo.

4Abiya akasimama juu ya Mlima Semaraimu, katika nchi ya vilima ya Efraimu, naye akasema, “Yeroboamu na Waisraeli wote, nisikilizeni!

5Hamfahamu kwamba Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, alimpa Daudi na wazao wake ufalme juu ya Israeli milele kwa agano la chumvi?

6Hata hivyo Yeroboamu mwana wa Nebati afisa wa Sulemani mwana wa Daudi, aliasi dhidi ya bwana wake.

7Baadhi ya watu wasiofaa kitu, wabaya kabisa walimkusanyikia na kumpinga Rehoboamu mwana wa Sulemani alipokuwa kijana mdogo asiyekuwa na uamuzi, asiye na nguvu za kuweza kupingana nao.

8“Hata sasa unapanga kupingana na ufalme wa Mwenyezi Mungu ambao uko mikononi mwa wazao wa Daudi. Kweli ninyi ni jeshi kubwa nanyi mnazo ndama za dhahabu Yeroboamu alizozitengeneza kuwa miungu yenu.

9Lakini je, hamkuwafukuza makuhani wa Mwenyezi Mungu, wana wa Haruni na Walawi na kujifanyia makuhani wenu wenyewe kama yafanyavyo mataifa ya nchi nyingine? Yeyote anayekuja kujiweka wakfu akiwa na ndama dume na kondoo dume saba aweza kuwa kuhani wa kile ambacho ni miungu kwenu.

10“Lakini kwetu sisi, Mwenyezi Mungu ndiye Mungu wetu, wala hatujamwacha. Makuhani wanaomtumikia Mwenyezi Mungu ni wana wa Haruni, nao Walawi wakiwasaidia.

11Kila asubuhi na jioni wao hutoa sadaka za kuteketezwa na kufukiza uvumba wa harufu nzuri kwa Mwenyezi Mungu. Wao huweka mikate juu ya meza takatifu, na kuwasha taa kwenye kinara cha dhahabu kila jioni. Sisi tunazishika kanuni za Mwenyezi Mungu, Mungu wetu. Lakini ninyi mmemwacha Mungu.

12Mungu yu pamoja nasi; yeye ndiye kiongozi wetu. Makuhani wake wakiwa na tarumbeta zao watapiga baragumu ya vita dhidi yenu. Watu wa Israeli, msipigane dhidi ya Mwenyezi Mungu, Mungu wa baba zenu, kwa maana hamtashinda.”

13Basi Yeroboamu alikuwa ametuma jeshi kuzunguka nyuma ya Yuda ili akiwa mbele ya Yuda, jeshi liwavizie kwa nyuma.

14Basi Yuda wakageuka na kuona kwamba wanashambuliwa mbele na nyuma. Ndipo wakamlilia Mwenyezi Mungu. Makuhani wakapiga tarumbeta zao,

15nao wanaume wa Yuda wakapiga ukelele wa vita. Walipopiga ukelele wa vita, Mungu akawafukuza Yeroboamu na Waisraeli wote mbele ya Mfalme Abiya na Yuda.

16Waisraeli wakakimbia mbele ya Yuda, naye Mungu akawatia mikononi mwao.

17Abiya na askari wake wakawachinja kwa machinjo makuu, hata wakawepo majeruhi elfu mia tano miongoni mwa watu wenye uwezo wa Israeli.

18Waisraeli walitiishwa katika tukio lile, nao watu wa Yuda wakawa washindi kwa sababu walimtegemea Mwenyezi Mungu, Mungu wa baba zao.

19Abiya akamfuatia Yeroboamu na kuteka miji ya Betheli, Yeshana na Efroni kutoka kwake, pamoja na vijiji vya miji hiyo.

20Yeroboamu hakupata nguvu tena wakati wa utawala wa Abiya. Naye Mwenyezi Mungu akampiga Yeroboamu akafa.

21Lakini Abiya akapata nguvu. Alioa wanawake kumi na wanne na alikuwa na wana ishirini na wawili na binti kumi na sita.

22Matukio mengine ya utawala wa Abiya, pamoja na mambo aliyofanya na aliyosema, yameandikwa katika kitabu cha maelezo cha nabii Ido.

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help