Ezra Utangulizi - Kiswahili Contemporary Scriptures 2024
UtanguliziVitabu vya Ezra na Nehemia vilikuwa kitabu kimoja katika Maandiko Matakatifu ya Kiebrania ambacho kilijulikana kama Ezra. Kitabu cha Ezra kinaeleza kuhusu kurudi kwa Wayahudi kutoka uhamishoni Babeli. Kinaanzia 539 K.K. na agizo alilotoa Koreshi, mfalme wa Uajemi, kwamba Waisraeli warudi Yerusalemu chini ya uongozi wa Zerubabeli. Agizo hili limetajwa katika milango miwili ya mwisho ya Mambo ya Nyakati. Watu walianza kujenga Hekalu kwa shauku na juhudi kubwa, na wakaanza kutoa dhabihu. Lakini kwa miaka 18 walicheleweshwa na adui zao kutoka kaskazini. Hatimaye mnamo 521 K.K. agizo kutoka kwa Dario mfalme wa Uajemi liliwapa nafasi ya kumalizia ujenzi huo. Walikamilisha kazi hiyo na kuweka Hekalu wakfu mnamo 516 K.K.Katika mwaka wa 458 K.K., Kuhani Ezra aliwasili Yerusalemu akiwa na kundi jingine la watu waliokuwa wamesalia uhamishoni huko Babeli. Aliwafundisha watu Torati ya Musa, na akarekebisha maisha yao ya kiroho ili mataifa yaliyowazunguka waweze kuona kwamba hili ni taifa lililochaguliwa na Mwenyezi Mungu.MwandishiInadhaniwa kwamba Ezra aliandika kitabu hiki.KusudiKuonesha uaminifu wa Mwenyezi Mungu, na jinsi alivyotimiza ahadi yake kwa kuwarejesha watu wake katika nchi yao.MahaliBabeli na Yerusalemu.TareheKama mwaka wa 450 K.K.Wahusika WakuuKoreshi, Zerubabeli, Hagai, Zekaria, Dario wa Kwanza, Artashasta wa Kwanza, na Ezra.Wazo KuuKuweka kumbukumbu ya mkusanyiko wa kwanza wa Israeli kitaifa baada ya kutawanyika miongoni mwa mataifa; pia kuonesha matatizo yanayoambatana na uhamisho wa kidini kuwiana na Torati ya Musa.Mambo MuhimuKurudi kwa Wayahudi kutoka uhamishoni; kujengwa upya kwa Hekalu; matatizo yaliyowakabili Waisraeli kutokana na kulijenga Hekalu tena.YaliyomoWatu wa kwanza kutoka uhamishoni Babeli na kurudi Yuda (1:1–2:70)Kujengwa kwa Hekalu na upinzani (3:1–6:22)Ezra arudi na kikundi cha pili kutoka Babeli, na marekebisho yake (7:1–10:44).