Warumi 10 - Kiswahili Contemporary Scriptures 2024

1Ndugu zangu, shauku ya moyo wangu na maombi yangu kwa Mungu ni kwa ajili ya Waisraeli, kwamba waokolewe.

2Kwa maana ninaweza nikashuhudia wazi kwamba wao wana juhudi kubwa kwa ajili ya Mungu, lakini juhudi yao haina maarifa.

3Kwa kuwa hawakuijua haki ya Mungu, wakatafuta kuweka haki yao wenyewe, hawakujitia chini ya haki ya Mungu.

4Kwa maana Al-Masihi ni ukomo wa sheria ili kila mtu aaminiye ahesabiwe haki.

Wokovu kwa watu wote

5Musa anaandika kuhusu haki ile itokanayo na sheria, kwamba, “Mtu atendaye matendo hayo ataishi kwa hayo.”

6Lakini ile haki itokanayo na imani husema hivi: “Usiseme moyoni mwako, ‘Ni nani atakayepanda mbinguni?’” (yaani ili kumleta Al-Masihi chini)

7“au ‘Ni nani atashuka kwenda Kuzimu?’” (yaani ili kumleta Al-Masihi kutoka kwa wafu).

8Lakini andiko lasemaje? “Lile neno liko karibu nawe, liko kinywani mwako na moyoni mwako,” yaani lile neno la imani tunalolihubiri.

9Kwa sababu, ukikiri kwa kinywa chako kwamba “Isa ni Bwana,” na kuamini moyoni mwako kwamba Mungu alimfufua kutoka kwa wafu, utaokoka.

10Kwa maana kwa moyo mtu huamini na hivyo kuhesabiwa haki, tena kwa kinywa mtu hukiri na hivyo kupata wokovu.

11Kama Maandiko yanavyosema, “Yeyote amwaminiye hataaibika kamwe.”

12Kwa maana hakuna tofauti kati ya Myahudi na mtu wa Mataifa, yeye ni Bwana wa wote, mwenye utajiri kwa wote wamwitao.

13Kwa maana, “Kila mtu atakayeliitia Jina la Mwenyezi Mungu, ataokolewa.”

14Lakini watamwitaje yeye ambaye hawajamwamini? Nao watawezaje kumwamini yeye ambaye hawajamsikia? Tena watamsikiaje bila mtu kuwahubiria?

15Nao watahubirije wasipopelekwa? Kama ilivyoandikwa, “Tazama jinsi ilivyo mizuri miguu yao wale wanaohubiri Habari Njema!”

16Lakini si wote waliotii Injili. Kwa maana Isaya asema, “Mwenyezi Mungu, ni nani aliyeamini ujumbe wetu?”

17Basi, imani chanzo chake ni kusikia, na kusikia huja kwa neno la Al-Masihi.

18Lakini nauliza: Je, wao hawakusikia? Naam, wamesikia, kwa maana:

“Sauti yao imeenea duniani pote,

nayo maneno yao yameenea

hadi miisho ya ulimwengu.”

19Nami nauliza tena: Je, Waisraeli hawakuelewa? Kwanza, Musa asema,

“Nitawafanya mwe na wivu

kwa watu wale ambao si taifa.

Nitawakasirisha kwa taifa

lile lisilo na ufahamu.”

20Naye Isaya kwa ujasiri mwingi anasema,

“Nimeonekana na watu wale ambao hawakunitafuta.

Nilijifunua kwa watu

wale ambao hawakunitafuta.”

21Lakini kuhusu Israeli anasema,

“Mchana kutwa nimewanyooshea

watu wakaidi na wasiotii mikono yangu.”

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help