1Mwenyezi Mungu akamwita Musa na kusema naye kutoka Hema la Kukutania, akamwambia,
2“Sema na Waisraeli, uwaambie, ‘Yeyote miongoni mwenu anayeleta sadaka kwa Mwenyezi Mungu, alete mnyama kama sadaka yake kutoka kundi lake la ng’ombe, au la kondoo na mbuzi.
3“ ‘Ikiwa sadaka hiyo ni sadaka ya kuteketezwa kutoka kundi la ng’ombe, atamtoa ng’ombe dume asiye na dosari. Ni lazima amlete kwenye ingilio la Hema la Kukutania ili aweze kukubalika kwa Mwenyezi Mungu.
4Ataweka mkono wake juu ya kichwa cha sadaka ya kuteketezwa, nayo itakubaliwa kwa niaba yake ili kufanya upatanisho kwa ajili yake.
5Atamchinja yule fahali mchanga mbele za Mwenyezi Mungu, kisha wana wa Haruni walio makuhani wataleta damu na kuinyunyiza pande zote za madhabahu yaliyo penye ingilio la Hema la Kukutania.
6Ataichuna hiyo sadaka ya kuteketezwa na kuikata vipande vipande.
7Wana wa Haruni kuhani wataweka moto juu ya madhabahu na kupanga kuni juu ya huo moto.
8Kisha hao wana wa Haruni walio makuhani watapanga vile vipande vya nyama, pamoja na kichwa na mafuta ya huyo mnyama, juu ya zile kuni zinazowaka juu ya madhabahu.
9Ataziosha sehemu za ndani za yule mnyama pamoja na miguu yake kwa maji; naye kuhani atavichoma vyote juu ya madhabahu. Hii ni sadaka ya kuteketezwa, sadaka iliyotolewa kwa moto, yenye harufu nzuri ya kumpendeza Mwenyezi Mungu.
10“ ‘Ikiwa sadaka ni sadaka ya kuteketezwa kutoka kundi la kondoo au mbuzi, atamtoa dume asiye na dosari.
11Atamchinjia upande wa kaskazini wa madhabahu mbele za Mwenyezi Mungu, nao wana wa Haruni walio makuhani watanyunyizia damu yake pande zote za madhabahu.
12Atamkata vipande vipande, naye kuhani atavipanga, pamoja na kichwa na mafuta ya mnyama juu ya zile kuni zinazowaka juu ya madhabahu.
13Ataosha sehemu za ndani na miguu kwa maji, naye kuhani atavileta vyote na kuvichoma juu ya madhabahu. Hii ni sadaka ya kuteketezwa, sadaka iliyotolewa kwa moto, harufu nzuri ya kumpendeza Mwenyezi Mungu.
14“ ‘Ikiwa sadaka inayotolewa kwa Mwenyezi Mungu ni sadaka ya kuteketezwa ya ndege, atamtoa hua au kinda la njiwa.
15Kuhani atamleta kwenye madhabahu, naye atamvunja shingo na kumnyofoa kichwa na kumchoma juu ya madhabahu. Damu yake itachuruzishwa ubavuni mwa madhabahu.
16Ataondoa kifuko cha chakula pamoja na uchafu wake na kuvitupa upande wa mashariki wa madhabahu, mahali pale penye majivu.
17Atampasua na kumweka wazi katika mabawa yake, lakini asimwachanishe kabisa, kisha kuhani ataichoma juu ya zile kuni zinazowaka juu ya madhabahu. Hii ni sadaka ya kuteketezwa, sadaka iliyotolewa kwa moto, harufu nzuri ya kumpendeza Mwenyezi Mungu.
Who We AreWhat We EelieveWhat We Do
2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.