Yohana 2 - Kiswahili Contemporary Scriptures 2024

Arusi huko Kana

1Siku ya tatu kulikuwa na arusi katika mji wa Kana ya Galilaya, naye mama yake Isa alikuwepo.

2Isa pamoja na wanafunzi wake walikuwa wamealikwa arusini pia.

3Divai ilipokwisha, mama yake Isa akamwambia, “Wameishiwa na divai.”

4Isa akamwambia, “Mama, kwa nini unanihusisha? Saa yangu haijawadia.”

5Mama yake akawaambia wale watumishi, “Fanyeni lolote atakalowaambia.”

6Basi hapo palikuwa na mitungi sita iliyotengenezwa kwa mawe; iliwekwa hapo kwa ajili ya desturi ya Kiyahudi ya kujitakasa; kila mtungi ungeweza kuchukua vipipa viwili au vitatu.

7Isa akawaambia wale watumishi, “Ijazeni hiyo mitungi maji.” Nao wakaijaza ile mitungi hadi juu.

8Kisha akawaambia, “Sasa choteni hayo maji kidogo; mpelekeeni mkuu wa sherehe.”

Hivyo wakachota, wakampelekea.

9Yule mkuu wa sherehe akayaonja yale maji ambayo yalikuwa yamebadilishwa kuwa divai. Hakujua divai hiyo ilikotoka ingawa wale watumishi waliochota yale maji walifahamu. Basi akamwita bwana arusi kando,

10akamwambia, “Watu wote hutoa divai nzuri kwanza, kisha huleta ile divai hafifu wageni wakisha kunywa sana; lakini wewe umeiweka ile nzuri zaidi hadi sasa.”

11Huu ndio muujiza wa kwanza wa Isa; aliufanya huko Kana ya Galilaya. Hivyo Isa alidhihirisha utukufu wake, nao wanafunzi wake wakamwamini.

12Baada ya hayo, Isa pamoja na mama yake, ndugu zake na wanafunzi wake, walishuka hadi Kapernaumu, wakakaa huko siku chache.

Isa atakasa Hekalu(Mathayo 21:12-17; Marko 11:15-17; Luka 19:45-48)

13Ilipokaribia wakati wa Pasaka ya Wayahudi, Isa alipanda kwenda Yerusalemu.

14Huko uani la Hekalu aliwakuta watu wakiuza ng’ombe, kondoo na njiwa, nao wengine walikuwa wameketi mezani wakibadili fedha.

15Akatengeneza mjeledi kutokana na kamba, akawafukuza wote kutoka ua la Hekalu, pamoja na kondoo na ng’ombe. Akazipindua meza za wale wabadili fedha na kuzimwaga fedha zao.

16Akawaambia wale waliokuwa wakiuza njiwa, “Waondoeni hapa! Mnathubutuje kuifanya nyumba ya Baba yangu kuwa mahali pa biashara?”

17Wanafunzi wake wakakumbuka kuwa imeandikwa: “Wivu wa nyumba yako utanila.”

18Ndipo Wayahudi wakamuuliza, “Unaweza kutuonesha ishara gani ili kuthibitisha mamlaka uliyo nayo ya kufanya mambo haya yote?”

19Isa akawajibu, “Libomoeni hili Hekalu, nami nitalijenga tena kwa siku tatu!”

20Wale Wayahudi wakamjibu, “Hekalu hili lilijengwa kwa muda wa miaka arobaini na sita, nawe wasema utalijenga kwa siku tatu?”

21Lakini yeye Hekalu alilozungumzia ni mwili wake.

22Baada ya kufufuliwa kutoka kwa wafu, wanafunzi wake wakakumbuka yale aliyokuwa amesema. Ndipo wakayaamini Maandiko na yale maneno Isa alikuwa ameyasema.

23Ikawa Isa alipokuwa Yerusalemu kwenye Sikukuu ya Pasaka, watu wengi waliona ishara na miujiza aliyokuwa akifanya, nao wakaamini katika jina lake.

24Lakini Isa hakujiaminisha kwao, kwa sababu aliwajua wanadamu wote.

25Hakuhitaji ushuhuda wa mtu yeyote kuhusu mwanadamu, kwa kuwa alijua yote yaliyokuwa moyoni mwa kila mtu.

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help