Waebrania Utangulizi - Kiswahili Contemporary Scriptures 2024
UtanguliziWaraka kwa Waebrania unajulikana kama kitabu cha mambo yaliyo bora, kwa sababu unazungumzia ukuu wa Al-Masihi na kumdhihirisha kama ufunuo wa mwisho wa Mwenyezi Mungu. Unabii na ahadi zilizoandikwa katika Maandiko Matakatifu zimetimizwa katika Injili, Al-Masihi akiwa Mpatanishi. Al-Masihi pia athibitishwa kuwa mkuu zaidi ya manabii, malaika, na Musa (ambaye alikuwa mpatanishi wa agano la hapo awali).Msomaji ameonywa asidharau wala kukataa wokovu mkuu uliotolewa kupitia kwake Al-Masihi. Uwezekano mkubwa ni kwamba waraka huu ulielekezwa kwa wafuasi wa Al-Masihi waliokuwa Wayahudi huko Palestina au Rumi, waliokuwa wanajaribiwa kugeukia tena dini ya Kiyahudi, au kuifanya Injili iwe yenye mfumo wa dini ya Kiyahudi.MwandishiIngawa waraka hauna jina la mwandishi, una ushahidi mwingi kwamba alikuwa mtu wa kizazi cha pili cha wafuasi wa Al-Masihi aliyekuwa na ujuzi sana wa Maandiko Matakatifu.KusudiMwandishi anamwonesha Isa kuwa ndiye ukamilifu wa ufunuo ulionenwa kwanza na Mwenyezi Mungu, na kisha na manabii wake.MahaliRumi.TareheKabla ya kuharibiwa kwa Hekalu huko Yerusalemu mnamo 70 B.K.Wahusika WakuuIsa, Yoshua, Musa, Melkizedeki, Ibrahimu, makuhani, malaika, na watu wenye imani wa zamani.Wazo KuuKiini cha Waebrania ni mamlaka na uweza wa Isa Al-Masihi kama Mjumbe wa neema ya Mwenyezi Mungu. Kitabu hiki kinatoa sifa za majina ya heshima zaidi ya ishirini yaliyomtaja Isa Al-Masihi katika huduma ya ukuhani na ya ufalme.Mambo MuhimuIsa Al-Masihi ni mng’ao wa utukufu wa Mwenyezi Mungu, na pia Al-Masihi ni mkuu kuliko malaika, mkuu kuliko viongozi wote, na mkuu kuliko makuhani.YaliyomoMnenaji bora kwa ajili ya Mwenyezi Mungu (1:1–4:13)Mwombezi au Kuhani aliye bora (4:14–7:28)Agano jipya na Dhabihu iliyo bora (8:1–10:18)Wito wa kuitunza na kuilinda imani (10:19–12:29)Kanuni za maisha ya wafuasi wa Al-Masihi, na maelezo ya binafsi (13:1-25).