Isaya 54 - Kiswahili Contemporary Scriptures 2024

Utukufu wa baadaye wa Sayuni

1“Imba, ewe mwanamke tasa,

wewe ambaye kamwe hukuzaa mtoto;

paza sauti kwa kuimba, piga kelele kwa furaha,

wewe ambaye kamwe hukupata uchungu;

kwa sababu watoto wa mwanamke aliyeachwa ukiwa ni wengi

kuliko wa mwanamke mwenye mume,”

asema Mwenyezi Mungu.

2“Panua mahali pa hema lako,

tandaza mapazia ya hema lako uyaeneze mbali,

wala usiyazuie;

ongeza urefu wa kamba zako,

imarisha vigingi vyako.

3Kwa maana utaenea upande wa kuume

na upande wa kushoto;

wazao wako watayamiliki mataifa

na kukaa katika miji yao iliyoachwa ukiwa.

4“Usiogope, wewe hutaaibika.

Usiogope aibu, wewe hutaaibishwa.

Wewe utasahau aibu ya ujana wako,

wala hutakumbuka tena mashutumu ya ujane wako.

5Kwa maana Muumba wako ndiye mume wako,

Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni ndilo jina lake,

yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli ni Mkombozi wako,

yeye anaitwa Mungu wa dunia yote.

6Mwenyezi Mungu atakuita urudi

kana kwamba ulikuwa mke aliyeachwa na kuhuzunishwa rohoni;

kama mke aliyeolewa bado angali kijana

na kukataliwa,” asema Mungu wako.

7“Kwa kitambo kidogo nilikuacha,

lakini kwa huruma nyingi nitakurudisha.

8Katika ukali wa hasira

nilikuficha uso wangu kwa kitambo,

lakini kwa fadhili za milele

nitakuwa na huruma juu yako,”

asema Mwenyezi Mungu Mkombozi wako.

9“Kwangu mimi jambo hili ni kama siku za Nuhu,

nilipoapa kuwa maji ya Nuhu kamwe hayatafunika tena dunia.

Hivyo sasa nimeapa sitawakasirikia ninyi,

kamwe sitawakemea tena.

10Ijapotikisika milima, na vilima viondolewe,

hata hivyo upendo wangu usiokoma kwenu hautatikisika,

wala agano langu la amani halitaondolewa,”

asema Mwenyezi Mungu, mwenye huruma juu yenu.

11“Ewe mji uliyeteswa, uliyepigwa kwa dhoruba

na usiyetulizwa,

nitakujenga kwa almasi,

nitaweka misingi yako

kwa yakuti samawi.

12Nitafanya minara yako ya akiki,

malango yako kwa vito ving’aavyo,

nazo kuta zako zote za vito vya thamani.

13Watoto wako wote watafundishwa na Mwenyezi Mungu,

nayo amani ya watoto wako itakuwa kuu.

14Kwa haki utathibitika:

Kuonewa kutakuwa mbali nawe;

hutaogopa chochote.

Hofu itakuwa mbali nawe;

haitakukaribia wewe.

15Kama mtu yeyote akikushambulia,

haitakuwa kwa ruhusa yangu;

yeyote akushambuliaye

atajisalimisha kwako.

16“Tazama, ni mimi niliyemuumba mhunzi,

yeye afukutaye makaa kuwa moto,

na kutengeneza silaha inayofaa kwa kazi yake.

Tena ni mimi niliyemwambia mharibu

kufanya uharibifu mwingi.

17Hakuna silaha itakayofanyizwa dhidi yako

itakayofanikiwa,

nawe utauthibitisha kuwa mwongo

kila ulimi utakaokushtaki.

Huu ndio urithi wa watumishi wa Mwenyezi Mungu

na hii ndiyo haki yao inayotoka kwangu,”

asema Mwenyezi Mungu.

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help