Waebrania 3 - Kiswahili Contemporary Scriptures 2024

Isa ni mkuu kuliko Musa

1Kwa hiyo ndugu watakatifu, mnaoshiriki mwito wa mbinguni, mtafakarini Isa, mtume na Kuhani Mkuu wa ukiri wetu.

2Alikuwa mwaminifu kwa yeye aliyemteua, kama Musa alivyokuwa mwaminifu katika nyumba yote ya Mungu.

3Isa ameonekana anastahili heshima kubwa kuliko Musa, kama vile mjenzi wa nyumba alivyo wa heshima kubwa kuliko nyumba yenyewe.

4Kwa kuwa kila nyumba hujengwa na mtu, lakini Mungu ni mjenzi wa kila kitu.

5Musa, kama mtumishi, alikuwa mwaminifu katika nyumba yote ya Mungu, akishuhudia kwa yale Mungu angeyasema baadaye.

6Lakini Al-Masihi ni mwaminifu kama Mwana katika nyumba ya Mungu. Sisi ndio nyumba yake, kama tutashikilia sana ujasiri wetu na tumaini tunalojivunia.

Onyo dhidi ya kutokuamini

7Kwa hiyo, kama Roho wa Mungu asemavyo:

“Leo, mkiisikia sauti yake,

8msiifanye mioyo yenu migumu,

kama mlivyofanya katika uasi,

wakati ule wa kujaribiwa jangwani,

9ambapo baba zenu walinijaribu na kunipima,

ingawa kwa miaka arobaini

walikuwa wameyaona matendo yangu.

10Hiyo ndiyo sababu nilikasirikia kizazi kile,

nami nikasema, ‘Siku zote mioyo yao imepotoka,

nao hawajazijua njia zangu.’

11Hivyo nikatangaza kwa kiapo katika hasira yangu,

‘Kamwe hawataingia rahani mwangu.’”

12Ndugu zangu, chungeni asiwepo miongoni mwenu mtu mwenye moyo mwovu usioamini, unaojitenga na Mungu aliye hai.

13Lakini mtiane moyo mtu na mwenzake kila siku, maadamu inaitwa “Leo”, ili asiwepo hata mmoja wenu mwenye kufanywa mgumu kwa udanganyifu wa dhambi.

14Kwa kuwa tumekuwa washiriki wa Al-Masihi, tukishikamana tu kwa uthabiti na tumaini letu la kwanza hadi mwisho.

15Kama ilivyonenwa:

“Leo, mkiisikia sauti yake,

msiifanye mioyo yenu migumu

kama mlivyofanya wakati wa kuasi.”

16Basi ni nani waliosikia lakini bado wakaasi? Je, si wale wote waliotoka Misri wakiongozwa na Musa?

17Lakini ni nani Mungu aliwakasirikia miaka arobaini? Je, si wale waliofanya dhambi ambao miili yao ilianguka jangwani?

18Ni nani hao ambao Mungu aliapa kuwa kamwe hawataingia rahani mwake isipokuwa ni wale waliokataa kutii?

19Hivyo tunaona kwamba hawakuweza kuingia kwa sababu ya kutokuamini kwao.

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help