1Yehoramu mwana wa Ahabu akawa mfalme wa Israeli katika Samaria mwaka wa kumi na nane wa utawala wa Yehoshafati mfalme wa Yuda, naye akatawala kwa miaka kumi na mbili.
2Akafanya maovu machoni pa Mwenyezi Mungu, lakini sio kama baba yake na mama yake walivyokuwa wamefanya. Akaondoa nguzo ya ibada ya Baali ambayo baba yake alikuwa ameitengeneza.
3Hata hivyo akashikamana na dhambi za Yeroboamu mwana wa Nebati, ambazo alisababisha Israeli kuzitenda, wala hakuziacha.
4Basi Mesha mfalme wa Moabu alikuwa mfuga kondoo; naye akatakiwa kumlipa mfalme wa Israeli ushuru wa wana-kondoo elfu mia moja, na sufu ya kondoo dume elfu mia moja.
5Lakini baada ya Ahabu kufa, mfalme wa Moabu aliasi dhidi ya mfalme wa Israeli.
6Kwa hiyo wakati ule Mfalme Yehoramu akaondoka kutoka Samaria na kukusanya Israeli yote tayari kwenda vitani.
7Akapeleka pia ujumbe ufuatao kwa Yehoshafati mfalme wa Yuda: “Mfalme wa Moabu ameasi dhidi yangu. Je, utaenda pamoja nami kupigana dhidi ya Moabu?”
Akajibu, “Nitaenda pamoja nawe. Mimi ni kama wewe, watu wangu ni kama watu wako, farasi wangu ni kama farasi wako.”
8Akauliza, “Je, tutashambulia kupitia njia gani?”
Akajibu, “Kupitia Jangwa la Edomu.”
9Hivyo mfalme wa Israeli akaondoka akiwa pamoja na mfalme wa Yuda na mfalme wa Edomu. Baada ya kuzunguka kwa siku saba, jeshi likawa limeishiwa maji kwa matumizi yao na kwa ajili ya wanyama waliokuwa nao.
10Mfalme wa Israeli akapaza sauti, akasema, “Nini! Je, Mwenyezi Mungu ametuita sisi wafalme watatu ili tu kututia mikononi mwa Moabu?”
11Lakini Yehoshafati akauliza, “Je, hayuko nabii wa Mwenyezi Mungu hapa, ili tuweze kumuuliza Mwenyezi Mungu kupitia kwake?”
Afisa mmoja wa mfalme wa Israeli akajibu, “Al-Yasa mwana wa Shafati yuko hapa. Ndiye alikuwa akimimina maji juu ya mikono ya Ilya.”
12Yehoshafati akasema, “Neno la Mwenyezi Mungu liko pamoja naye.” Kwa hiyo mfalme wa Israeli na Yehoshafati pamoja na mfalme wa Edomu wakamwendea.
13Al-Yasa akamwambia mfalme wa Israeli, “Nina uhusiano gani nawe? Nenda kwa manabii wa baba yako na manabii wa mama yako.”
Mfalme wa Israeli akajibu, “La, sivyo, kwa sababu ni Mwenyezi Mungu ametuita pamoja sisi wafalme watatu ili atutie mikononi mwa Moabu.”
14Al-Yasa akasema, “Hakika kama Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni aishivyo, ninayemtumikia, kama si kwa heshima niliyo nayo kwa Yehoshafati mfalme wa Yuda, nisingekujali hata kidogo.
15Lakini sasa, nileteeni mpiga kinubi.”
Mpiga kinubi alipokuwa akipiga, mkono wa Mwenyezi Mungu ukaja juu ya Al-Yasa,
16naye akasema, “Hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu, ‘Chimbeni bonde hili lijae mahandaki.’
17Kwa kuwa hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu: Hamtaona upepo wala mvua, lakini bonde hili litajaa maji, nanyi pamoja na ng’ombe wenu na wanyama wenu wengine mtakunywa.
18Hili ni jambo rahisi machoni pa Mwenyezi Mungu. Pia ataitia Moabu mikononi mwenu.
19Mtaushinda kila mji wenye ngome na kila mji mkubwa. Mtakata kila mti ulio mzuri, mtaziba chemchemi zote, na kuharibu kila shamba zuri kwa mawe.”
20Kesho yake asubuhi, karibu na wakati wa kutoa dhabihu ya asubuhi, tazama, maji yakawa yanatiririka kutoka upande wa Edomu! Nayo nchi ikajaa maji.
21Basi Wamoabu wote walikuwa wamesikia kuwa wale wafalme wamekuja kupigana dhidi yao. Hivyo kila mtu, kijana na mzee, ambaye angeweza kushika silaha akaitwa na kuwekwa mpakani.
22Walipoamka asubuhi na mapema, jua likawa linamulika juu ya maji. Wamoabu waliokuwa upande wa pili wakaona maji ni mekundu, kama damu.
23Wamoabu wakasema, “Ile ni damu! Lazima hao wafalme wamepigana na kuchinjana wao kwa wao. Sasa Moabu, twendeni tukateke nyara!”
24Lakini Wamoabu walipofika kwenye kambi ya Israeli, Waisraeli wakainuka na kuwapiga hata wakakimbia. Nao Waisraeli wakaivamia nchi na kuwachinja Wamoabu.
25Wakaiharibu miji, kila mtu akatupa jiwe juu ya kila shamba zuri hadi likafunikwa. Wakaziba chemchemi zote na kukata kila mti mzuri. Kir-Haresethi peke yake ndio uliobaki na mawe yake yakiwa mahali pake. Lakini hata hivyo watu waliokuwa na makombeo wakauzunguka na kuushambulia.
26Mfalme wa Moabu alipoona kuwa vita vimekuwa vikali dhidi yake, akachukua watu mia saba wenye panga ili kuingia kwa mfalme wa Edomu, lakini wakashindwa.
27Ndipo akamchukua mwanawe mzaliwa wake wa kwanza, ambaye angekuwa mfalme baada yake, akamtoa kama dhabihu ya kuteketezwa juu ya ukuta wa mji. Ghadhabu ikawa kubwa dhidi ya Israeli; wakajiondoa kwake na kurudi katika nchi yao wenyewe.
Who We AreWhat We EelieveWhat We Do
2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.