Isaya 31 - Kiswahili Contemporary Scriptures 2024

Ole wa wale wanaotegemea Misri

1Ole wao wale wanaoshuka Misri kutafuta msaada,

wale wanaotegemea farasi,

wanaoweka tumaini katika wingi wa magari yao ya vita,

na katika nguvu nyingi za wapanda farasi,

lakini hawamwangalii yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli,

wala hawatafuti msaada kwa Mwenyezi Mungu.

2Hata hivyo yeye pia ana hekima na anaweza kuleta maafa,

wala hayatangui maneno yake.

Yeye atainuka dhidi ya nyumba ya mwovu,

dhidi ya wale ambao huwasaidia watenda maovu.

3Lakini Wamisri ni wanadamu, wala si Mungu,

farasi wao ni nyama, wala si roho.

Mwenyezi Mungu atakaponyoosha Mkono wake,

yeye anayesaidia atajikwaa,

naye anayesaidiwa ataanguka,

wote wawili wataangamia pamoja.

4Hili ndilo Mwenyezi Mungu analoniambia:

“Kama vile simba angurumavyo,

simba mkubwa juu ya mawindo yake:

hata ingawa kundi lote la wafugaji

huitwa pamoja dhidi yake,

hatiwi hofu na kelele zao,

wala kusumbuliwa na ghasia zao;

ndivyo Mwenyezi Mungu,

Mungu wa majeshi ya mbinguni atakavyoshuka

kufanya vita juu ya Mlima Sayuni

na juu ya vilele vyake.

5Kama ndege warukao,

Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni

ataukinga Yerusalemu;

ataukinga na kuuokoa,

atapita juu yake na kuufanya salama.”

6Mrudieni yeye ambaye nyumba ya Israeli imemwasi sana.

7Kwa kuwa katika siku ile kila mmoja wenu atazikataa sanamu za fedha na za dhahabu zilizotengenezwa kwa mikono yenu yenye dhambi.

8“Ashuru itaanguka kwa upanga ambao si wa mwanadamu;

upanga usio wa kibinadamu utawaangamiza.

Watakimbia mbele ya upanga

na vijana wao wa kiume watafanyizwa kazi kwa lazima.

9Ngome zao zitaanguka kwa sababu ya hofu;

kwa kuona bendera ya vita,

majemadari wao watashikwa na hofu ya ghafula,”

asema Mwenyezi Mungu,

ambaye moto wake uko Sayuni,

nalo tanuru lake liko Yerusalemu.

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help