Waefeso 6 - Kiswahili Contemporary Scriptures 2024

Mafundisho kuhusu watoto na wazazi

1Enyi watoto, watiini wazazi wenu katika Bwana Isa, kwa kuwa hili ni jema.

2“Waheshimu baba yako na mama yako,” hii ndio amri ya kwanza yenye ahadi,

3“upate baraka na uishi siku nyingi duniani.”

4Ninyi akina baba, msiwachokoze watoto wenu, bali waleeni kwa nidhamu na mafundisho ya Bwana Isa.

Mafundisho kuhusu watumwa na mabwana

5Ninyi watumwa, watiini hao walio mabwana zenu hapa duniani kwa heshima na kwa kutetemeka na kwa unyofu wa moyo, kama vile mnavyomtii Al-Masihi.

6Watiini, si tu wakati wakiwaona ili mpate upendeleo wao, bali mtumike kama watumwa wa Al-Masihi, mkifanya mapenzi ya Mungu kwa moyo.

7Tumikeni kwa moyo wote, kama vile mngemtumikia, wala si wanadamu,

8mkijua kwamba Bwana Isa atampa kila mtu thawabu kwa lolote jema alilotenda, awe mtumwa au mtu huru.

9Nanyi mabwana, watendeeni watumwa wenu kwa jinsi hiyo hiyo. Msiwatishe, kwa kuwa mnajua kwamba yeye aliye Bwana wenu na Bwana wao yuko mbinguni, naye hana upendeleo.

Silaha za Mwenyezi Mungu

10Hatimaye, mzidi kuwa hodari katika Bwana Isa na katika uweza wa nguvu zake.

11Vaeni silaha zote za Mungu ili mweze kuzipinga hila za ibilisi.

12Kwa maana kushindana kwetu si dhidi ya mwili na damu, bali dhidi ya falme na mamlaka, dhidi ya wakuu wa ulimwengu huu wa giza na majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho.

13Kwa hiyo vaeni silaha zote za Mungu ili mweze kushindana siku ya uovu itakapokuja, nanyi mkiisha kufanya yote, simameni imara.

14Kwa hiyo simameni imara mkiwa mmejifunga kweli kiunoni na kuvaa dirii ya haki kifuani,

15nayo miguu yenu ivalishwe viatu vya utayari tunaopata katika Injili ya amani.

16Zaidi ya haya yote, twaeni ngao ya imani, ambayo kwa hiyo mtaweza kuizima mishale yote yenye moto ya yule mwovu.

17Vaeni chapeo ya wokovu na mchukue upanga wa Roho wa Mungu, ambao ni neno la Mungu,

18mkiomba kwa Roho siku zote katika sala zote na maombi, mkikesha kila wakati mkiwaombea watakatifu wote.

19Niombeeni na mimi pia, ili kila nifunguapo kinywa changu, nipewe maneno ya kusema, niweze kutangaza siri ya Injili kwa ujasiri,

20ambayo mimi ni balozi wake katika vifungo. Ombeni ili nipate kuhubiri kwa ujasiri kama inipasavyo.

Salamu za mwisho

21Tikiko, aliye ndugu mpendwa na mtumishi mwaminifu katika Bwana Isa, atawaambia kila kitu, ili pia mpate kujua hali yangu na kile ninachofanya.

22Ninamtuma kwenu kwa ajili ya kusudi hili hasa, ili mpate kujua hali yetu, na awatie moyo.

23Amani iwe kwa ndugu, na pendo pamoja na imani kutoka kwa Mungu Baba Mwenyezi na kwa Bwana Isa Al-Masihi.

24Neema iwe na wote wanaompenda Bwana wetu Isa Al-Masihi kwa upendo wa dhati. Amen.

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help