Hesabu 17 - Kiswahili Contemporary Scriptures 2024

Kuchipuka kwa fimbo ya Haruni

1Mwenyezi Mungu akamwambia Musa,

2“Sema na Waisraeli, na ujipatie fimbo kumi na mbili kutoka kwao, moja kutoka kwa kila mmoja wa viongozi wa makabila ya baba zao. Andika jina la kila mtu kwenye fimbo yake.

3Kwenye fimbo ya Lawi andika jina la Haruni, kwa maana ni lazima iwepo fimbo moja kwa kila kiongozi kwa ajili ya kila kabila la baba zao.

4Ziweke hizo fimbo ndani ya Hema la Kukutania mbele ya Sanduku la Ushuhuda, mahali nikutanapo nawe.

5Fimbo ya mtu nitakayemchagua itachipuka, nami mwenyewe nitayakomesha haya manung’uniko ya mara kwa mara ya Waisraeli dhidi yako.”

6Hivyo Musa akasema na Waisraeli, nao viongozi wao wakampa fimbo kumi na mbili, fimbo moja kwa ajili ya kila kabila la baba zao, nayo fimbo ya Haruni ikiwa miongoni mwa hizo.

7Musa akaziweka hizo fimbo mbele za Mwenyezi Mungu ndani ya Hema la Ushuhuda.

8Siku iliyofuata Musa aliingia kwenye Hema la Ushuhuda akaona ile fimbo ya Haruni ambayo iliwakilisha jamaa ya Lawi haikuwa tu imechipuka, bali pia ilikuwa imetoa machipukizi, kuchanua maua na kuzaa malozi.

9Ndipo Musa akaleta zile fimbo zote kwa Waisraeli wote kutoka mbele za Mwenyezi Mungu. Wakaziangalia, na kila mtu akaichukua fimbo yake mwenyewe.

10Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Rudisha fimbo ya Haruni mbele ya Sanduku la Ushuhuda, ili ihifadhiwe kama alama kwa waasi. Hili litakomesha manung’uniko yao dhidi yangu, ili wasife.”

11Musa akafanya kama Mwenyezi Mungu alivyomwamuru.

12Waisraeli wakamwambia Musa, “Tutakufa! Tumepotea, sote tumepotea!

13Yeyote akaribiaye Maskani ya Mwenyezi Mungu atakufa. Je, sisi sote tutakufa?”

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help