Kumbukumbu 18 - Kiswahili Contemporary Scriptures 2024

Sadaka kwa makuhani na Walawi

1Makuhani ambao ni Walawi, yaani kabila lote la Lawi, hawatakuwa na mgawo wala urithi pamoja na Israeli. Wataishi kwa sadaka zitolewazo kwa ajili ya Mwenyezi Mungu za kuteketezwa kwa moto, kwa maana huo ndio urithi wao.

2Hawatakuwa na urithi miongoni mwa ndugu zao; Mwenyezi Mungu ndiye urithi wao, kama alivyowaahidi.

3Hili ndilo fungu la makuhani kutoka kwa watu watakaotoa dhabihu ya fahali au kondoo: mguu wa mbele, mataya na matumbo.

4Mtawapa malimbuko ya nafaka zenu, divai mpya, mafuta na sufu ya kwanza kutoka manyoya ya kondoo wenu,

5kwa kuwa Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, amewachagua pamoja na wazao wao kutoka makabila yenu kusimama na kuhudumu katika jina la Mwenyezi Mungu siku zote.

6Ikiwa Mlawi atahama kutoka mojawapo ya miji yenu popote katika Israeli ambapo anaishi, akaja kwa moyo wote mahali Mwenyezi Mungu atakapopachagua,

7anaweza akahudumu katika jina la Mwenyezi Mungu, Mungu wake, kama Walawi wenzake wote wanaohudumu hapo mbele za Mwenyezi Mungu.

8Atashiriki sawa katika mafao yao, hata kama amepokea fedha kutoka mauzo ya mali ya jamaa yake.

Matendo ya machukizo

9Mtakapoingia katika nchi ambayo Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, anawapa, msijifunze kuiga njia za machukizo za mataifa ya huko.

10Asionekane mtu yeyote miongoni mwenu ampitishaye mwanawe au binti yake katika moto, atakayefanya uaguzi, ulozi, anayetabiri nyakati, anayejishughulisha na uchawi,

11wala arogaye kwa kupiga mafundo, wala mwaguzi au anayeabudu mizimu, wala awaombaye wafu.

12Mtu yeyote afanyaye mambo haya ni chukizo kwa Mwenyezi Mungu, tena ni kwa sababu ya matendo haya ya kuchukiza wayafanyayo ndiyo maana Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, atayafukuza mataifa hayo mbele yenu.

13Kamwe msilaumiwe mbele za Mwenyezi Mungu, Mungu wenu.

Nabii

14Mataifa mtakayowafukuza husikiliza wale wafanyao ulozi na uaguzi. Lakini ninyi, Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, hajawaruhusu kufanya hivyo.

15Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, atawainulia nabii kama mimi kutoka miongoni mwa ndugu zenu wenyewe. Msikilizeni yeye.

16Kwa kuwa hivi ndivyo mlivyomwomba Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, kule Horebu siku ile ya kusanyiko, wakati mliposema, “Na tusiisikie sauti ya Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, wala kuuona moto huu mkubwa tena, ama sivyo tutakufa.”

17Mwenyezi Mungu akaniambia: “Wanachosema ni vyema.

18Nitawainulia nabii kama wewe kutoka miongoni mwa ndugu zao; nitaweka maneno yangu kinywani mwake, naye atawaambia kila kitu nitakachomwamuru.

19Kama mtu yeyote hatasikiliza maneno yangu ambayo huyo nabii atayasema kwa Jina langu, mimi mwenyewe nitamwajibisha.

20Lakini nabii ambaye atathubutu kusema kwa Jina langu kitu chochote ambacho sikumwamuru akiseme, au nabii ambaye husema kwa jina la miungu mingine ni lazima auawe.”

21Mnaweza kuulizana wenyewe, “Tutawezaje kujua wakati ujumbe haukusemwa na Mwenyezi Mungu?”

22Ikiwa kile nabii anachotangaza kwa jina la Mwenyezi Mungu hakikutendeka au kutimia, huo ni ujumbe ambao Mwenyezi Mungu hakusema. Nabii huyo amesema kwa ujuaji. Msimwogope huyo.

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help