1Baada ya kifo cha Mfalme Ahabu, nchi ya Moabu iliasi dhidi ya Israeli.
2Basi Ahazia alikuwa ameanguka huko Samaria kutoka baraza ya chumba chake cha juu, akaumia. Hivyo akatuma wajumbe, akiwaambia, “Nendeni mkaulize kwa Baal-Zebubu, mungu wa Ekroni, mkaone kama nitapona kutokana na kuumia huku.”
3Lakini malaika wa Mwenyezi Mungu akamwambia Ilya Mtishbi, “Panda uende ukakutane na wajumbe wa mfalme wa Samaria, uwaulize, ‘Je, ni kwa sababu hakuna Mungu katika Israeli ndiyo maana mnaenda kumuuliza Baal-Zebubu, mungu wa Ekroni?’
4Kwa hiyo hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, ‘Hutaondoka kwenye kitanda unachokilalia. Hakika utakufa!’ ” Hivyo Ilya akaenda.
5Wajumbe waliporudi kwa mfalme, akawauliza, “Kwa nini mmerudi?”
6Wakamjibu, “Mtu mmoja alikuja kukutana nasi, naye akatuambia, ‘Rudini kwa mfalme aliyewatuma na mkamwambie, “Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: Je, ni kwa sababu hakuna Mungu katika Israeli ndiyo maana unawatuma watu kwenda kuuliza kwa Baal-Zebubu, mungu wa Ekroni? Kwa hiyo hutaondoka kwenye kitanda unachokilalia. Hakika utakufa!” ’ ”
7Mfalme akawauliza, “Alikuwa mtu wa namna gani ambaye mlikutana naye, akawaambia hili?”
8Wakamjibu, “Alikuwa mtu aliyekuwa na vazi la manyoya na mkanda wa ngozi kiunoni mwake.”
Mfalme akasema, “Huyo alikuwa ni Ilya Mtishbi.”
9Ndipo mfalme akamtuma mkuu mmoja wa kikosi pamoja na kikosi chake cha askari hamsini kwa nabii Ilya. Yule mkuu wa kikosi akamwendea Ilya, aliyekuwa ameketi juu ya kilima, na kumwambia, “Mtu wa Mungu, mfalme anasema, ‘Shuka chini!’ ”
10Ilya akamjibu yule mkuu wa kikosi, “Ikiwa mimi ni mtu wa Mungu, moto na ushuke kutoka mbinguni ukuteketeze wewe na watu wako hamsini!” Ndipo moto ukashuka kutoka mbinguni na kuwateketeza yule mkuu wa kikosi pamoja na watu wake.
11Aliposikia hili, mfalme akatuma kwa Ilya mkuu wa kikosi mwingine na askari wake hamsini. Yule mkuu wa kikosi akamwambia Ilya, “Mtu wa Mungu, hili ndilo asemalo mfalme, ‘Shuka chini mara moja!’ ”
12Ilya akajibu, “Ikiwa mimi ni mtu wa Mungu, moto na ushuke kutoka mbinguni ukuteketeze wewe na watu wako hamsini!” Ndipo moto wa Mungu ukashuka kutoka mbinguni, ukamteketeza yeye na watu wake hamsini.
13Hivyo mfalme akatuma mkuu wa kikosi wa tatu na watu wake hamsini. Huyu mkuu wa kikosi wa tatu akapanda na kupiga magoti mbele ya Ilya, akiomba, “Mtu wa Mungu, tafadhali niachie uhai wangu na uhai wa hawa watu hamsini, watumishi wako!
14Tazama, moto umeshuka kutoka mbinguni na kuwateketeza wale wakuu wa vikosi viwili vya kwanza pamoja na watu wao. Lakini sasa niachie uhai wangu!”
15Malaika wa Mwenyezi Mungu akamwambia Ilya, “Shuka pamoja naye, usimwogope.” Hivyo Ilya akainuka na kushuka pamoja naye kwa mfalme.
16Akamwambia mfalme, “Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: Je, ni kwa sababu hakuna Mungu katika Israeli wa kumuuliza habari, ndiyo maana ukatuma wajumbe kuuliza Baal-Zebubu, mungu wa Ekroni? Kwa sababu umefanya hili, kamwe hutaondoka kwenye kitanda unachokilalia. Hakika utakufa!”
17Hivyo akafa, sawasawa na lile neno la Mwenyezi Mungu ambalo Ilya alikuwa amesema.
Kwa kuwa Ahazia hakuwa na mwana, Yoramu akawa mfalme baada yake katika mwaka wa pili wa Yehoramu mwana wa Yehoshafati mfalme wa Yuda.
18Kuhusu matukio mengine ya utawala wa Ahazia na yale aliyoyafanya, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Israeli?
Who We AreWhat We EelieveWhat We Do
2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.