Amosi 3 - Kiswahili Contemporary Scriptures 2024

Mashahidi waitwa dhidi ya Israeli

1Sikilizeni neno hili alilosema Mwenyezi Mungu dhidi yenu, enyi watu wa Israeli, dhidi ya jamaa nzima niliowapandisha toka Misri:

2“Ni ninyi tu niliowachagua

kati ya jamaa zote za dunia;

kwa hiyo nitawaadhibu

kwa ajili ya dhambi zenu zote.”

3Je, watu wawili hutembea pamoja

wasipokubaliana kufanya hivyo?

4Je, simba hunguruma katika kichaka

wakati hana mawindo?

Aweza kuvuma katika pango

wakati ambao hajakamata chochote?

5Je, ndege aweza kuanguka kwenye mtego ulio ardhini

ambapo hajategewa chambo?

Je, mtego unaweza kufyatuka toka ardhini

wakati hakuna chochote cha kunasa?

6Je, tarumbeta inapopigwa mjini kujulisha hatari,

watu hawatetemeki?

Mji unapopatwa na maafa,

je, si Mwenyezi Mungu amesababisha?

7Hakika Bwana Mungu Mwenyezi hatafanya neno lolote

bila kuwafunulia watumishi wake manabii siri yake.

8Simba amenguruma:

je, ni nani ambaye hataogopa?

Bwana Mungu Mwenyezi ametamka:

je, ni nani awezaye kukosa kutoa unabii?

9Tangazeni katika ngome za Ashdodi

na katika ngome za Misri:

“Kusanyikeni juu ya milima ya Samaria;

angalieni wingi wa wasiwasi ulio ndani yake,

na uonevu ulio miongoni mwa watu wake.”

10Mwenyezi Mungu asema: “Hawajui kutenda lililo jema,

wale ambao hujilundikia nyara

na vitu vilivyotekwa katika ngome zao.”

11Kwa hiyo hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi:

“Adui ataizingira nchi;

ataangusha chini ngome zenu

na kuteka nyara maboma yenu.”

12Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu:

“Kama vile mchungaji aokoavyo kinywani mwa simba

vipande viwili tu vya mfupa wa mguu

au kipande cha sikio,

hivyo ndivyo Waisraeli watakavyookolewa,

wale wanaokaa Samaria

kwenye kingo za vitanda vyao,

na katika Dameski

kwenye viti vyao vya fahari.”

13“Sikia hili na ushuhudie dhidi ya nyumba ya Yakobo,” asema Bwana, yeye Bwana Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni.

14“Siku nitakapomwadhibu Israeli kwa sababu ya dhambi zake,

nitaharibu madhabahu za Betheli;

pembe za madhabahu zitakatiliwa mbali

na kuanguka chini.

15Nitabomoa nyumba ya wakati wa masika,

pamoja na nyumba ya wakati wa kiangazi;

nyumba zilizonakshiwa kwa pembe za ndovu

na majumba makubwa ya fahari yatabomolewa,”

asema Mwenyezi Mungu.

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help