Isaya 23 - Kiswahili Contemporary Scriptures 2024

Unabii kuhusu Tiro

1Neno la unabii kuhusu Tiro:

Ombolezeni, enyi meli za Tarshishi!

Kwa kuwa Tiro imeangamizwa,

imeachwa bila nyumba wala bandari.

Kuanzia nchi ya Kitimu

neno limewajia.

2Nyamazeni kimya, enyi watu wa kisiwani,

pia ninyi wafanyabiashara wa Sidoni,

ambao mabaharia wamewatajirisha.

3Kwenye maji makuu

nafaka za Shihori zilikuja;

mavuno ya Mto Naili yalikuwa mapato ya Tiro,

naye akawa soko la mataifa.

4Uaibishwe ee Sidoni, nawe ee ngome la bahari,

kwa kuwa bahari imesema:

“Sijapata kuwa na uchungu wa kuzaa wala sijapata kuzaa,

wala sijapata kulea wana wala kutunza binti.”

5Habari ifikapo Misri,

watakuwa katika maumivu makuu kwa ajili ya taarifa kutoka Tiro.

6Vukeni hadi Tarshishi,

ombolezeni, enyi watu wa kisiwani.

7Je, huu ndio mji wenu uliojaa sherehe,

mji wa zamani, zamani kabisa

ambao miguu yake imeuchukua

kufanya makao nchi za mbali sana?

8Ni nani amepanga hili dhidi ya Tiro,

mji utoao mataji,

ambao wafanyabiashara wake ni wana wa mfalme

na wachuuzi wake ni watu mashuhuri wa dunia?

9Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni ndiye alipanga jambo hili,

ili kukishusha kiburi cha utukufu wote

na kuwanyenyekeza wale wote

ambao ni mashuhuri duniani.

10Ee Binti Tarshishi,

pita katika nchi yako kama vile Mto Naili

kwa kuwa huna tena bandari.

11Mwenyezi Mungu amenyoosha mkono wake juu ya bahari

na kuzifanya falme zake zitetemeke.

Ametoa amri kuhusu Kanaani

kwamba ngome zake ziangamizwe.

12Alisema, “Usizidi kufurahi,

ee Bikira Binti Sidoni, sasa umepondwa!

“Simama, vuka uende Kitimu;

hata huko hutapata pumziko.”

13Tazama katika nchi ya Wakaldayo,

watu hawa ambao sasa hawaonekani kama wapo!

Waashuru wameifanya nchi hiyo

kuwa mahali pa viumbe wa jangwani.

Wamesimamisha minara yao ya kuuzingira,

wameziteka ngome zake na kuziacha tupu

na kuufanya kuwa magofu.

14Ombolezeni, enyi meli za Tarshishi;

ngome yenu imeangamizwa!

15Wakati huo Tiro utasahauliwa kwa miaka sabini, muda wa maisha ya mfalme. Lakini mwisho wa miaka hiyo sabini, itakuwa kwa Tiro kama ilivyo katika wimbo wa kahaba:

16“Twaa kinubi, tembea mjini kote,

ewe kahaba uliyesahauliwa;

piga kinubi vizuri, imba nyimbo nyingi,

ili upate kukumbukwa.”

17Mwishoni mwa miaka sabini, Mwenyezi Mungu atatembelea Tiro. Naye Tiro atarudia ajira yake ya ukahaba, na atafanya biashara yake na falme zote duniani.

18Lakini faida na mapato yake yatawekwa wakfu kwa Mwenyezi Mungu; hayatahifadhiwa wala kufichwa. Faida zake zitaenda kwa wale wanaoishi mbele za Mwenyezi Mungu kwa ajili ya chakula tele na mavazi mazuri.

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help