Zaburi 44 - Kiswahili Contemporary Scriptures 2024

Zaburi 44Kuomba ulinzi wa Mwenyezi MunguKwa mwimbishaji. Utenzi wa wana wa Kora.

1Ee Mungu, tumesikia kwa masikio yetu,

baba zetu wametueleza

yale uliyotenda katika siku zao,

siku za kale.

2Kwa mkono wako uliwafukuza mataifa

na ukawapanda baba zetu,

uliangamiza mataifa

na kuwastawisha baba zetu.

3Sio kwa upanga wao waliipata nchi,

wala si mkono wao uliwapatia ushindi;

ilikuwa ni kitanga cha mkono wako wa kuume,

na nuru ya uso wako,

kwa kuwa uliwapenda.

4Wewe ni mfalme wangu na Mungu wangu,

unayeamuru ushindi kwa Yakobo.

5Kwa uwezo wako tunawasukuma nyuma watesi wetu;

kwa jina lako tunawakanyaga adui zetu.

6Siutumaini upinde wangu,

upanga wangu hauniletei ushindi;

7bali wewe unatupatia ushindi juu ya adui zetu,

unawaaibisha watesi wetu.

8Katika Mungu wetu tunajivuna mchana kutwa,

nasi tutalisifu jina lako milele.

9Lakini sasa umetukataa na kutudhili,

wala huendi tena na jeshi letu.

10Umetufanya tukimbie mbele ya adui,

nao watesi wetu wametuteka nyara.

11Umetuacha tutafunwe kama kondoo

na umetutawanya katika mataifa.

12Umewauza watu wako kwa fedha kidogo,

wala hukupata faida yoyote kwa mauzo yao.

13Umetufanya lawama kwa majirani zetu,

dharau na dhihaka kwa wale wanaotuzunguka.

14Umetufanya kuwa mithali miongoni mwa mataifa;

mataifa hututikisia vichwa vyao.

15Fedheha yangu iko mbele yangu mchana kutwa,

na uso wangu umejaa aibu tele,

16kwa ajili ya dhihaka ya wale wanaonilaumu na kunitukana,

kwa sababu ya adui, ambaye anatamani kulipiza kisasi.

17Hayo yote yametutokea,

ingawa tulikuwa hatujakusahau

wala hatujaenda kinyume na agano lako.

18Mioyo yetu ilikuwa haijarudi nyuma;

nyayo zetu zilikuwa hazijaiacha njia yako.

19Lakini ulituponda na kutufanya makao ya mbweha,

na ukatufunika kwa giza nene.

20Kama tungekuwa tumelisahau jina la Mungu wetu

au kunyooshea mikono yetu kwa mungu mgeni,

21je, si Mungu angegundua hili,

kwa kuwa anazijua siri za moyo?

22Hata hivyo kwa ajili yako tunauawa mchana kutwa;

tumehesabiwa kama kondoo wa kuchinjwa.

23Amka, Ee Bwana! Kwa nini unalala?

Zinduka! Usitukatae milele.

24Kwa nini unauficha uso wako

na kusahau taabu na mateso yetu?

25Tumeshushwa hadi mavumbini,

miili yetu imegandamana na ardhi.

26Inuka na utusaidie,

utukomboe kwa sababu ya upendo wako usio na mwisho.

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help