Zaburi 92 - Kiswahili Contemporary Scriptures 2024

Zaburi 92Wimbo wa kumsifu Mwenyezi MunguZaburi. Wimbo wa siku ya Sabato.

1Ni vyema kumshukuru Mwenyezi Mungu

na kuliimbia jina lako, Ee Uliye Juu Sana,

2kuutangaza upendo wako asubuhi,

na uaminifu wako wakati wa usiku,

3kwa zeze yenye nyuzi kumi

na kwa sauti ya kinubi.

4Ee Mwenyezi Mungu, kwa kuwa matendo yako yamenifurahisha,

nitaziimba kwa shangwe kazi za mikono yako.

5Ee Mwenyezi Mungu, tazama jinsi yalivyo makuu matendo yako,

tazama jinsi yalivyo ya kina mawazo yako!

6Mjinga hafahamu,

mpumbavu haelewi,

7ingawa waovu huchipua kama majani

na wote watendao maovu wanastawi,

wataangamizwa milele.

8Bali wewe, Ee Mwenyezi Mungu,

utatukuzwa milele.

9Ee Mwenyezi Mungu, hakika adui zako,

hakika adui zako wataangamia.

Wote watendao maovu watatawanyika.

10Umeitukuza pembe yangu kama ile ya nyati dume,

mafuta mazuri yamemiminwa juu yangu.

11Macho yangu yamewaona adui zangu wakishindwa,

masikio yangu yamesikia maangamizi ya adui zangu waovu.

12Wenye haki watastawi kama mtende,

watakuwa kama mwerezi wa Lebanoni,

13waliopandwa katika nyumba ya Mwenyezi Mungu,

watastawi katika nyua za Mungu wetu.

14Wakati wa uzee watakuwa bado wanazaa matunda,

watakuwa wabichi tena wamejaa nguvu,

15wakitangaza, “Mwenyezi Mungu ni mkamilifu;

yeye ni Mwamba wangu,

na ndani yake hamna uovu.”

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help