Zaburi 39 - Kiswahili Contemporary Scriptures 2024

Zaburi 39Maombi ya mtu mwenye uchunguKwa mwimbishaji. Mtindo wa Yeduthuni. Zaburi ya Daudi.

1Nilisema, “Nitaziangalia njia zangu

na kuuzuia ulimi wangu usije ukatenda dhambi;

nitaweka lijamu kinywani mwangu

wakati wote waovu wanapokuwa karibu nami.”

2Lakini niliponyamaza na kutulia,

hata pasipo kusema lolote jema,

uchungu wangu uliongezeka.

3Moyo wangu ulipata moto ndani yangu,

nilipotafakari, moto uliwaka,

ndipo nikasema kwa ulimi wangu:

4“Ee Mwenyezi Mungu, nijulishe mwisho wa maisha yangu

na hesabu ya siku zangu;

nijalie kujua jinsi maisha yangu

yanavyopita upesi.

5Umefanya maisha yangu mafupi kama nyanda;

muda wangu wa kuishi ni kama

hauna thamani kwako.

Maisha ya kila mwanadamu

ni kama pumzi.

6Hakika kila binadamu ni kama njozi

aendapo huku na huko:

hujishughulisha na mengi, lakini ni ubatili;

anakusanya mali nyingi,

wala hajui ni nani atakayejifaidi nayo.

7“Lakini sasa Bwana, nitafute nini?

Tumaini langu ni kwako.

8Niokoe kutoka makosa yangu yote,

usinifanye kuwa dhihaka ya wapumbavu.

9Nilinyamaza, sikufumbua kinywa changu,

kwa sababu wewe ndiwe uliyetenda hili.

10Niondolee mjeledi wako,

nimeshindwa kwa mapigo ya mkono wako.

11Unakemea na kuadhibu wanadamu

kwa ajili ya dhambi zao;

unaharibu utajiri wao kama nondo aharibuvyo:

kila mwanadamu ni kama pumzi tu.

12“Ee Mwenyezi Mungu, usikie maombi yangu,

usikie kilio changu unisaidie,

usiwe kiziwi kwa kulia kwangu.

Kwani mimi ninaishi na wewe kama mgeni,

mhamiaji, kama walivyokuwa baba zangu wote,

13Tazama mbali nami, ili niweze kufurahi tena

kabla sijaondoka na nisiwepo tena.”

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help