1watu wote wakakusanyika kama mtu mmoja kwenye uwanja mbele ya Lango la Maji. Wakamwambia Ezra mwandishi alete Kitabu cha Torati ya Musa, ambacho Mwenyezi Mungu aliamuru kwa ajili ya Israeli.
2Basi katika siku ya kwanza ya mwezi wa saba, kuhani Ezra akaleta Torati mbele ya kusanyiko, ambamo walikuwamo wanaume, wanawake na watu wote walioweza kufahamu.
3Akaisoma kwa sauti kubwa tangu mapambazuko hadi adhuhuri, akiwa ameuelekea uwanja uliokuwa mbele ya Lango la Maji mbele ya wanaume, wanawake na wengine ambao waliweza kufahamu. Watu wote wakasikiliza kwa makini kile Kitabu cha Torati.
4Mwandishi Ezra alikuwa amesimama juu ya jukwaa la miti lililojengwa kwa kusudi hilo. Karibu naye upande wa kuume walisimama Matithia, Shema, Anaya, Uria, Hilkia na Maaseya. Upande wake wa kushoto walikuwa Pedaya, Mishaeli, Malkiya, Hashumu, Hashbadani, Zekaria na Meshulamu.
5Ezra akakifungua kile kitabu. Watu wote waliweza kumwona kwa sababu alikuwa amesimama juu zaidi, naye alipokifungua watu wote wakasimama.
6Ezra akamsifu Mwenyezi Mungu, Mungu mkuu, nao watu wote wakainua mikono yao na kuitikia, “Amen! Amen!” Kisha wakasujudu na kumwabudu Mwenyezi Mungu, nyuso zao zikigusa chini.
7Watu wakiwa wamesimama pale, Walawi wafuatao waliwafundisha ile Torati: Yeshua, Bani, Sherebia, Yamini, Akubu, Shabethai, Hodia, Maaseya, Kelita, Azaria, Yozabadi, Hanani na Pelaya.
8Walisoma kutoka kile Kitabu cha Torati ya Mungu, wakiifafanua na kuwapa maelezo ili watu waweze kufahamu kile kilichokuwa kikisomwa.
9Ndipo Nehemia aliyekuwa mtawala, Ezra kuhani na mwandishi, pamoja na Walawi waliokuwa wakiwafundisha watu wakawaambia wote, “Siku hii ni takatifu kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wenu. Msiomboleze wala msilie.” Kwa kuwa watu wote walikuwa wakilia walipokuwa wakisikiliza maneno ya ile Torati.
10Nehemia akasema, “Nendeni mkafurahie chakula kizuri na vinywaji vitamu, na mpeleke sehemu kwa wale ambao hawana chochote cha kula. Siku hii ni takatifu kwa Mwenyezi Mungu. Msihuzunike, kwa kuwa furaha ya Mwenyezi Mungu ni nguvu zenu.”
11Walawi wakawatuliza watu wote wakisema, “Kuweni watulivu, kwa kuwa hii ni siku takatifu. Msihuzunike.”
12Kisha watu wote wakaondoka kwenda kula na kunywa, na kupeana sehemu ya chakula, na wakaadhimisha kwa furaha kubwa, kwa sababu sasa walifahamu maneno yale waliyokuwa wameelezwa.
13Katika siku ya pili ya mwezi, wakuu wa jamaa zote, pamoja na makuhani na Walawi, walikusanyika wakimzunguka Ezra mwandishi ili wapate kusikiliza kwa makini maneno ya Torati.
14Wakakuta imeandikwa katika ile Torati, ambayo Mwenyezi Mungu aliiamuru kupitia kwa Musa, kwamba Waisraeli walipaswa kukaa katika vibanda wakati wa sikukuu ya mwezi wa saba,
15na kwamba walipaswa kutangaza neno hili na kulieneza katika miji yao na katika Yerusalemu wakisema: “Nendeni katika nchi ya vilima na kuleta matawi kutoka miti ya mizeituni, mizeituni mwitu, mihadasi, mitende na miti ya kivuli, ili kutengeneza vibanda,” kama ilivyoandikwa.
16Basi watu wakaenda na kuleta matawi, nao wakajijengea vibanda juu ya paa za nyumba zao, katika nyua zao, katika nyua za nyumba ya Mungu, na katika uwanja karibu na Lango la Maji, na uwanja wa Lango la Efraimu.
17Jamii yote ya watu waliorudi kutoka utumwani wakajenga vibanda na kuishi ndani yake. Tangu wakati wa Yoshua mwana wa Nuni hadi siku ile, Waisraeli hawakuwahi kuiadhimisha namna hii. Furaha yao ilikuwa kubwa sana.
18Siku baada ya siku, kuanzia siku ya kwanza hadi ya mwisho, Ezra alisoma katika kile Kitabu cha Torati ya Mungu. Wakaiadhimisha sikukuu ile kwa siku saba, nayo siku ya nane, kufuatana na maagizo, kulikuwa na kusanyiko maalum.
Who We AreWhat We EelieveWhat We Do
2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.