Zaburi 55 - Kiswahili Contemporary Scriptures 2024

Zaburi 55Maombi ya mtu aliyesalitiwa na rafikiKwa mwimbishaji. Na ala za uimbaji. Utenzi wa Daudi.

1Ee Mungu, sikiliza maombi yangu,

wala usidharau hoja yangu.

2Nisikie na unijibu.

Mawazo yangu yananisumbua na nimehangaishwa

3kwa sauti ya adui,

kwa kukaziwa macho na waovu,

kwa sababu wananiletea mateso juu yangu

na kunitukana kwa hasira zao.

4Moyo wangu umejaa uchungu,

hofu za mauti zimenishambulia.

5Woga na kutetemeka vimenizunguka,

hofu kuu imenigharikisha.

6Nilisema, “Laiti ningekuwa na mabawa ya njiwa!

Ningeruka niende mbali kupumzika.

7Ningetorokea mbali sana

na kukaa jangwani,

8ningeharakisha kwenda mahali pa salama,

mbali na tufani kali na dhoruba.”

9Ee Bwana, uwatahayarishe waovu

na uwachanganyishie semi zao,

maana nimeona jeuri na ugomvi mjini.

10Usiku na mchana wanazunguka juu ya kuta zake,

uovu na dhuluma vimo ndani yake.

11Nguvu za uharibifu zinatenda kazi mjini,

vitisho na uongo haviondoki mitaani mwake.

12Kama aliyenitukana ni adui yangu, ningevumilia,

kama mtu mwovu angejiinua dhidi yangu,

ningejificha asinione.

13Kumbe ni wewe, mwenzangu,

mshiriki na rafiki yangu wa karibu,

14ambaye awali tulifurahia ushirika mzuri,

tulipokuwa tukienda na umati hekaluni mwa Mungu.

15Kifo na kiwajie adui zangu ghafula,

na washuke Kuzimu wangali hai,

kwa maana uovu uko ndani yao.

16Lakini ninamwita Mungu,

naye Mwenyezi Mungu huniokoa.

17Jioni, asubuhi na adhuhuri

ninalia kwa huzuni,

naye husikia sauti yangu.

18Huniokoa nikawa salama katika vita

vilivyopangwa dhidi yangu,

ingawa watu wengi hunipinga.

19Mungu anayemiliki milele,

atawasikia na kuwaadhibu,

watu ambao hawabadilishi njia zao,

wala hawana hofu ya Mungu.

20Mwenzangu hushambulia rafiki zake,

naye huvunja agano lake.

21Mazungumzo yake ni laini kama siagi,

hata hivyo vita vimo moyoni mwake.

Maneno yake ni mororo kuliko mafuta,

hata hivyo ni upanga mkali uliofutwa.

22Mtwike Mwenyezi Mungu fadhaa zako,

naye atakutegemeza,

hatamwacha kamwe mwenye haki wake aanguke.

23Lakini wewe, Ee Mungu,

utawashusha waovu katika shimo la uharibifu.

Wenye kiu ya kumwaga damu na wenye hila,

hawataishi nusu ya siku zao.

Lakini mimi ninakutumaini wewe.

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help