Ufunuo 4 - Kiswahili Contemporary Scriptures 2024

Kiti cha enzi mbinguni

1Baada ya mambo hayo nilitazama, nami nikaona mbele yangu mlango uliokuwa wazi mbinguni. Nayo ile sauti niliyokuwa nimeisikia hapo mwanzo ikisema nami kama tarumbeta ikasema, “Njoo huku, nami nitakuonesha yale ambayo hayana budi kutendeka baada ya haya.”

2Ghafula nilikuwa katika Roho wa Mungu, na hapo mbele yangu palikuwa kiti cha enzi mbinguni, kikiwa kimekaliwa na mtu.

3Aliyekuwa amekikalia alikuwa anaonekana kama yaspi na akiki. Kukizunguka kile kiti cha enzi palikuwa na upinde wa mvua uliong’aa kama zumaridi.

4Kukizunguka hicho kiti cha enzi palikuwa na viti vingine ishirini na vinne vya utawala, na juu ya hivyo viti walikuwa wameketi wazee ishirini na wanne. Walivaa mavazi meupe, na walikuwa na taji za dhahabu vichwani mwao.

5Kwenye kile kiti cha enzi palikuwa panatoka miali ya radi, ngurumo na sauti za radi. Mbele ya kiti cha enzi, taa saba zilikuwa zinawaka. Hizi ndizo roho saba za Mungu.

6Pia mbele ya kiti cha enzi palikuwa na kile kilichoonekana kama bahari ya kioo, iliyokuwa angavu kama bilauri.

Katikati, kukizunguka kile kiti cha enzi, kulikuwa na viumbe wanne wenye uhai, wamejaa macho mbele na nyuma.

7Kiumbe wa kwanza mwenye uhai alikuwa kama simba, wa pili alikuwa kama ng’ombe dume, wa tatu alikuwa na uso kama wa mwanadamu, na wa nne alikuwa kama tai anayeruka.

8Kila mmoja wa hawa viumbe wanne wenye uhai alikuwa na mabawa sita, na kujawa na macho pande zote hadi chini ya mabawa. Usiku na mchana hawaachi kusema:

“Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu,

ni Bwana Mungu Mwenyezi,

aliyekuwako, aliyeko, na atakayekuja.”

9Kila mara viumbe hao wanne wenye uhai wanapomtukuza, kumheshimu na kumshukuru yeye aliyeketi kwenye kile kiti cha enzi, tena aishiye milele na milele,

10wale wazee ishirini na wanne huanguka mbele zake aliyeketi kwenye kiti cha enzi, na kumwabudu yeye aliye hai milele na milele. Huziweka taji zao mbele ya kiti cha enzi, wakisema:

11“Bwana wetu na Mungu wetu,

wewe unastahili kupokea utukufu

na heshima na uweza,

kwa maana ndiwe uliyeviumba vitu vyote,

na kwa mapenzi yako viliumbwa

na vimekuwako.”

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help