Zaburi 91 - Kiswahili Contemporary Scriptures 2024

Zaburi 91Mwenyezi Mungu mlinzi wetu

1Yeye akaaye mahali pa salama pake Yeye Aliye Juu Sana,

atadumu katika uvuli wake Mwenyezi.

2Nitasema kumhusu Mwenyezi Mungu, “Yeye ndiye kimbilio langu na ngome yangu,

Mungu wangu, ninayemtumaini.”

3Hakika yeye ataniokoa na mtego wa mwindaji,

na maradhi ya kuambukiza ya kuua.

4Atakufunika kwa manyoya yake,

chini ya mabawa yake utapata kimbilio,

uaminifu wake utakuwa ngao na kinga yako.

5Hutaogopa vitisho vya usiku,

wala mshale urukao mchana,

6wala maradhi ya kuambukiza

yanayonyemelea gizani,

wala tauni iharibuyo adhuhuri.

7Ijapo watu elfu wataangukia kando yako,

kumi elfu mkono wako wa kuume,

lakini haitakukaribia wewe.

8Utatazama tu kwa macho yako

na kuona adhabu ya waovu.

9Ukimfanya Aliye Juu Sana kuwa makao yako;

naam, Mwenyezi Mungu ambaye ni kimbilio langu;

10basi hakuna madhara yatakayokupata wewe,

hakuna maafa yatalikaribia hema lako.

11Kwa kuwa atawaagiza malaika wake kwa ajili yako,

wakulinde katika njia zako zote.

12Watakuchukua mikononi mwao,

ili usijikwae mguu wako kwenye jiwe.

13Utawakanyaga simba na nyoka wakali,

simba mkubwa na nyoka utawaponda kwa miguu.

14Mwenyezi Mungu asema, “Kwa kuwa ananipenda, nitamwokoa;

nitamlinda, kwa kuwa analikiri Jina langu.

15Ataniita, nami nitamjibu;

nitakuwa pamoja naye katika taabu,

nitamwokoa na kumheshimu.

16Kwa siku nyingi nitamshibisha

na kumwonesha wokovu wangu.”

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help