Ayubu 17 - Kiswahili Contemporary Scriptures 2024

1Moyo wangu umevunjika,

siku zangu zimefupishwa,

kaburi linaningojea.

2Hakika wenye mizaha wamenizunguka;

macho yangu yamebaki kutazama uadui wao.

Ayubu anaomba msaada

3“Ee Mungu, nipe dhamana unayodai.

Ni nani mwingine atakayeweka dhamana kwa ajili yangu?

4Umezifunga akili zao zisipate ufahamu,

kwa hiyo hutawaacha wapate ushindi.

5Kama mtu akiwashutumu rafiki zake ili apate ujira,

macho ya watoto wake yatashindwa kuona.

6“Mungu amenifanya kitu cha dhihaka kwa kila mtu,

mtu ambaye watu humtemea mate usoni.

7Macho yangu yamefifia kwa ajili ya majonzi;

umbile langu lote ni kama kivuli.

8Watu wanyofu wanatishwa na hili;

watu wasio na hatia wanasimama dhidi ya wasiomcha Mungu.

9Hata hivyo, waadilifu watazishika njia zao,

nao wale wenye mikono safi wataendelea kupata nguvu.

10“Lakini ninyi njooni, ninyi nyote, jaribuni tena!

Sitampata mtu mwenye hekima miongoni mwenu.

11Siku zangu zimepita, mipango yangu imevunjika,

vivyo hivyo shauku za moyo wangu.

12Watu hawa hufanya usiku kuwa mchana,

kwenye giza wao husema, ‘Mwanga u karibu.’

13Kama nyumba pekee ninayoitarajia ni kaburi,

nikikitandika kitanda changu gizani,

14nikiuambia uharibifu, ‘Wewe u baba yangu,’

na kuliambia buu, ‘Wewe u mama yangu’ au ‘Dada yangu,’

15liko wapi basi tarajio langu?

Ni nani awezaye kuona tarajio lolote kwa ajili yangu?

16Je, litashuka chini hadi kwenye malango ya mauti?

Je, tutashuka pamoja mavumbini?”

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help