Amosi 6 - Kiswahili Contemporary Scriptures 2024

Ole kwa wanaoridhika

1Ole wenu ninyi mnaostarehe na kuridhika katika Sayuni,

na ninyi mnaojisikia salama juu ya Mlima Samaria,

ninyi watu mashuhuri wa taifa lililoendelea kuliko mataifa mengine,

ambao watu wa Israeli wanawategemea!

2Nendeni Kalne mkaone kutoka huko;

mwende hadi Hamathi iliyo kuu,

kisha mshuke hadi Gathi ya Wafilisti.

Je, wao ni bora kuliko falme zenu mbili?

Je, nchi yao ni kubwa kuliko yenu?

3Mnaiweka mbali siku iliyo mbaya

na kuleta karibu utawala wa kuogofya.

4Ninyi mnalala juu ya vitanda vilivyofunikwa kwa pembe za ndovu,

na kujinyoosha juu ya viti vya fahari.

Mnajilisha kwa wana-kondoo wazuri

na ndama walionenepeshwa.

5Ninyi mnapiga vinubi kama Daudi,

huku mkitunga nyimbo za vinanda mbalimbali.

6Mnakunywa mvinyo kwa bakuli zilizojazwa,

na mnajipaka mafuta mazuri,

lakini hamhuzuniki kwa maangamizi ya Yusufu.

7Kwa hiyo mtakuwa miongoni mwa watu wa kwanza kwenda uhamishoni;

karamu zenu na kustarehe kutakoma.

Mwenyezi Mungu anachukia kiburi cha Israeli

8Bwana Mungu Mwenyezi ameapa kwa nafsi yake mwenyewe: Bwana Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, asema:

“Nachukia kiburi cha Yakobo,

nachukia ngome zake;

nitautoa mji wao na kila kitu

kilicho ndani yake.”

9Kama watu kumi watabaki katika nyumba moja, wao pia watakufa.

10Kama jamaa ambaye atachoma miili akija ili kuitoa nje ya nyumba, na kumuuliza yeyote ambaye bado anajificha humo, “Je, yuko mtu yeyote pamoja nawe?” Naye akisema, “Hapana,” ndipo atakaposema, “Nyamaza! Haturuhusiwi kutaja jina la Mwenyezi Mungu.”

11Kwa kuwa Mwenyezi Mungu ameamuru,

naye atabomoa jumba kubwa vipande vipande

na nyumba ndogo vipande vidogo vidogo.

12Je, farasi wanaweza kukimbia

kwenye miamba iliyochongoka?

Je, mtu aweza kulima kwa maksai huko?

Lakini mmegeuza haki kuwa sumu

na matunda ya uadilifu kuwa uchungu:

13ninyi mnaoshangilia kushindwa kwa Lo-Debari

na kusema, “Je, hatukuteka Karnaimu

kwa nguvu zetu wenyewe?”

14Maana Bwana Mwenyezi Mungu,

Mungu wa majeshi ya mbinguni, asema,

“Nitainua taifa dhidi yenu, ee nyumba ya Israeli,

nalo litawatesa kuanzia Lebo-Hamathi

hadi Bonde la Araba.”

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help