1Neno la unabii kuhusu Misri:
Tazama, Mwenyezi Mungu amepanda juu ya wingu liendalo kwa haraka
naye anakuja Misri.
Sanamu za Misri zinatetemeka mbele yake,
nayo mioyo ya Wamisri inayeyuka ndani yao.
2“Nitamchochea Mmisri dhidi ya Mmisri,
ndugu atapigana dhidi ya ndugu,
jirani dhidi ya jirani,
mji dhidi ya mji,
ufalme dhidi ya ufalme.
3Wamisri watakufa moyo,
na nitaibatilisha mipango yao.
Watatafuta ushauri kwa sanamu na kwa roho za waliokufa,
kwa waaguzi na kwa wale waongeao na mizimu.
4Nitawatia Wamisri
mikononi mwa bwana mkatili
na mfalme mkali atawatawala,”
asema Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni.
5Maji ya mito yatakauka,
chini ya mto kutakauka kwa jua.
6Mifereji itanuka;
vijito vya Misri vitapungua
na kukauka.
Matete na nyasi vitanyauka,
7pia mimea iliyo kando ya Mto Naili,
pale mto unapomwaga maji baharini.
Kila shamba lililopandwa kando ya Mto Naili litakauka,
litapeperushwa na kutoweka kabisa.
8Wavuvi watalia na kuomboleza,
wote watupao ndoana katika Mto Naili,
na watupao nyavu katika maji
watadhoofika kwa majonzi.
9Wale watu wafanyao kazi ya kitani kilichochambuliwa watakata tamaa,
wafumaji wa kitani safi watavunjika moyo.
10Wafanyao kazi ya kufuma nguo watahuzunishwa,
nao vibarua wataugua moyoni.
11Maafisa wa Soani ni wapumbavu kabisa,
washauri wa Farao wenye busara wanatoa ushauri wa kijinga.
Unawezaje kumwambia Farao,
“Mimi ni mmoja wa watu wenye hekima,
mwanafunzi wa wafalme wa zamani”?
12Wako wapi sasa watu wako wenye hekima?
Wao wakuoneshe na kukufahamisha
ni nini Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni
amepanga dhidi ya Misri.
13Maafisa wa Soani wamekuwa wapumbavu,
viongozi wa Memfisi wamedanganyika,
walio mawe ya pembe ya taifa lake
wameipotosha Misri.
14Mwenyezi Mungu amewamwagia
roho ya kizunguzungu;
wanaifanya Misri iyumbayumbe
katika yale yote inayoyafanya,
kama vile mlevi ayumbayumbavyo
katika kutapika kwake.
15Misri haiwezi kufanya kitu chochote,
cha kichwa wala cha mkia,
cha tawi la mtende wala cha tete.
16Katika siku ile Wamisri watakuwa kama wanawake. Watatetemeka kwa hofu mbele ya mkono wa Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni anaoinua dhidi yao.
17Nayo nchi ya Yuda itawatia hofu Wamisri, kila mmoja atakayetajiwa Yuda ataingiwa na hofu, kwa sababu ya kile ambacho Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni anapanga dhidi yao.
18Katika siku hiyo miji mitano ya Misri, itazungumza lugha ya Kanaani, na kuapa kumtii Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni. Mji mmoja utaitwa Mji wa Uharibifu.
19Katika siku hiyo patakuwa na madhabahu ya Mwenyezi Mungu katikati ya Misri na mnara wa kumbukumbu kwa Mwenyezi Mungu kwenye mpaka wa Misri.
20Itakuwa alama na ushahidi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni katika nchi ya Misri. Watakapomlilia Mwenyezi Mungu kwa sababu ya watesi wao, Mungu atawapelekea mwokozi na mtetezi, naye atawaokoa.
21Hivyo Mwenyezi Mungu atajijulisha mwenyewe kwa Wamisri, nao katika siku hiyo watamkubali Mwenyezi Mungu. Wataabudu kwa kumtolea dhabihu na sadaka za nafaka, watamwekea Mwenyezi Mungu nadhiri na kuzitimiza.
22Mwenyezi Mungu ataipiga Misri kwa tauni; atawapiga na kuwaponya. Watamgeukia Mwenyezi Mungu, naye atayasikia maombi yao na kuwaponya.
23Katika siku hiyo kutakuwa na njia kuu kutoka Misri hadi Ashuru. Waashuru wataenda Misri, na Wamisri wataenda Ashuru. Wamisri na Waashuru wataabudu pamoja.
24Katika siku hiyo Israeli itakuwa ya tatu, pamoja na Misri na Ashuru, nao watakuwa baraka kwa dunia.
25Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni atawabariki, akisema, “Baraka iwe kwa Misri watu wangu, kwa Ashuru kazi ya mikono yangu, na kwa Israeli urithi wangu.”
Who We AreWhat We EelieveWhat We Do
2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.