Yohana 7 - Kiswahili Contemporary Scriptures 2024

Kutokuamini kwa ndugu zake Isa

1Baada ya mambo haya, Isa alienda sehemu mbalimbali za Galilaya. Hakutaka kwenda Yudea kwa sababu viongozi wa Wayahudi huko walitaka kumuua.

2Sikukuu ya Vibanda ya Wayahudi ilikuwa imekaribia.

3Hivyo ndugu zake Isa wakamwambia, “Ondoka hapa uende Yudea ili wanafunzi Wako wapate kuona miujiza unayofanya.

4Mtu anayetaka kujulikana hafanyi mambo yake kwa siri. Kama unafanya mambo haya, jioneshe kwa ulimwengu.”

5Hata ndugu zake mwenyewe hawakumwamini.

6Isa akawaambia, “Wakati wangu bado haujawadia, lakini wakati wenu upo siku zote.

7Ulimwengu hauwezi kuwachukia ninyi, lakini unanichukia mimi kwa sababu ninawashuhudia kwamba matendo yao ni maovu.

8Ninyi nendeni kwenye Sikukuu, lakini mimi sitahudhuria Sikukuu hii kwa sababu wakati wangu haujawadia.”

9Baada ya kusema hayo, akabaki Galilaya.

Isa kwenye Sikukuu ya Vibanda

10Lakini ndugu zake walipokwisha kuondoka kwenda kwenye Sikukuu, yeye pia alienda lakini kwa siri.

11Viongozi wa Wayahudi walikuwa wakimtafuta huko kwenye Sikukuu na kuulizana, “Yuko wapi huyu mtu?”

12Kulikuwa na minong’ono iliyoenea kumhusu Isa katika umati wa watu, wakati wengine wakisema, “Ni mtu mwema.”

Wengine walikuwa wakisema, “La, yeye anawadanganya watu.”

13Lakini hakuna mtu yeyote aliyemsema waziwazi kwa sababu ya kuwaogopa viongozi wa Wayahudi.

Isa afundisha kwenye Sikukuu

14Ilipokaribia katikati ya Sikukuu, Isa alipanda kwenda Hekaluni na kuanza kufundisha.

15Wayahudi wakastaajabia mafundisho yake wakasema, “Mtu huyu amepataje kujua mambo haya bila kufundishwa?”

16Ndipo Isa akawajibu, “Mafundisho yangu si yangu mwenyewe, bali yanatoka kwake yeye aliyenituma.

17Mtu yeyote akipenda kufanya mapenzi ya Mungu, atajua kama mafundisho yangu yanatoka kwa Mungu au ninasema kwa ajili yangu mwenyewe.

18Wale wanenao kwa ajili yao wenyewe hufanya hivyo kwa kutaka utukufu wao wenyewe. Lakini yeye atafutaye utukufu wa yule aliyemtuma ni wa kweli, wala hakuna uongo ndani yake.

19Je, Musa hakuwapa ninyi sheria? Lakini hakuna hata mmoja wenu anayeishika hiyo sheria. Kwa nini mnataka kuniua?”

20Ule umati wa watu wakamjibu, “Wewe una pepo mchafu! Ni nani anayetaka kukuua?”

21Isa akawajibu, “Nimefanya muujiza mmoja na nyote mkastaajabu.

22Lakini kwa kuwa Musa aliwaamuru tohara (ingawa kwa kweli haikutoka kwa Musa bali kwa baba zetu wa zamani), mnamtahiri mtoto hata siku ya Sabato.

23Ikiwa mtoto aweza kutahiriwa siku ya Sabato kusudi Torati ya Musa isivunjwe, kwa nini mnanikasirikia kwa kumponya mtu mwili wake wote siku ya Sabato?

24Acheni kuhukumu mambo kwa jinsi mnavyoona tu, bali hukumuni kwa haki.”

Je, Isa ndiye Al-Masihi?

25Ndipo baadhi ya watu wa Yerusalemu wakawa wanasema, “Tazameni, huyu si yule mtu wanayetaka kumuua?

26Mbona yuko hapa anazungumza hadharani, na wala hawamwambii neno lolote? Je, inawezekana viongozi wanafahamu kuwa huyu ndiye Al-Masihi?

27Tunafahamu huyu mtu anakotoka, lakini Al-Masihi atakapokuja, hakuna yeyote atakayejua atokako.”

28Ndipo Isa, akaendelea kufundisha Hekaluni, akisema, “Ninyi mnanifahamu na kujua nitokako. Mimi sikuja kwa ajili yangu mwenyewe, bali yeye aliyenituma ni wa kweli na ninyi hammjui.

29Mimi namjua kwa kuwa nimetoka kwake, naye ndiye alinituma.”

30Ndipo wakatafuta kumkamata, lakini hakuna mtu yeyote aliyethubutu kumshika kwa sababu saa yake ilikuwa bado haijawadia.

31Nao watu wengi wakamwamini, wakasema, “Je, Al-Masihi atakapokuja, atafanya miujiza mikuu kuliko aliyoifanya mtu huyu?”

Walinzi wanatumwa kumkamata Isa

32Mafarisayo wakasikia watu wakinong’ona mambo kama hayo kuhusu Isa, ndipo wao pamoja na viongozi wa makuhani wakatuma walinzi wa Hekalu waende kumkamata.

33Isa akasema, “Mimi bado niko pamoja nanyi kwa kitambo kidogo, kisha nitarudi kwake yeye aliyenituma.

34Mtanitafuta lakini hamtaniona, nami niliko ninyi hamwezi kuja.”

35Wayahudi wakaulizana wao kwa wao, “Huyu mtu anataka kwenda wapi ambako hatuwezi kumfuata? Je, anataka kwenda kwa Wayunani ambako baadhi ya watu wetu wametawanyikia, akawafundishe Wayunani?

36Yeye ana maana gani anaposema, ‘Mtanitafuta lakini hamtaniona,’ na, ‘nami niliko ninyi hamwezi kuja’?”

Mito ya maji ya uzima

37Siku ile ya mwisho ya Sikukuu, siku ile kuu, wakati Isa akiwa amesimama huko, akapaza sauti yake akasema, “Kama mtu yeyote anaona kiu na aje kwangu anywe.

38Yeyote aniaminiye mimi, kama Maandiko yanavyosema, vijito vya maji ya uzima vitatiririka kutoka ndani yake.”

39Isa aliposema haya, alimaanisha Roho Mtakatifu wa Mungu, ambaye wote waliomwamini wangempokea. Kwa maana hadi wakati huo Roho wa Mungu alikuwa hajatolewa, kwa kuwa Isa alikuwa bado hajatukuzwa.

Mgawanyiko miongoni mwa watu

40Waliposikia maneno hayo, baadhi ya watu miongoni mwa umati ule wakasema, “Hakika huyu ndiye yule Nabii.”

41Wengine wakasema, “Huyu ndiye Al-Masihi!”

Lakini wengine wakauliza, “Je, Al-Masihi kwao ni Galilaya?

42Je, Maandiko hayasemi kwamba Al-Masihi atakuja kutoka jamaa ya Daudi na kutoka Bethlehemu, mji alioishi Daudi?”

43Kwa hiyo watu wakagawanyika kwa ajili ya Isa.

44Baadhi yao walitaka kumkamata, lakini hakuna aliyethubutu kumgusa.

Kutokuamini kwa viongozi wa Wayahudi

45Hatimaye wale walinzi wa Hekalu wakarudi kwa viongozi wa makuhani na Mafarisayo waliokuwa wamewatuma ili kumkamata Isa, wakaulizwa, “Mbona hamkumkamata?”

46Wale walinzi wakajibu, “Kamwe hajanena mtu yeyote kama yeye anenavyo.”

47Mafarisayo wakajibu, “Je, nanyi pia mmedanganyika?

48Je, kuna kiongozi yeyote au mmoja wa Mafarisayo ambaye amemwamini?

49Lakini umati huu wa watu wasiojua Torati ya Musa, wamelaaniwa.”

50Ndipo Nikodemo, yule aliyekuwa amemwendea Isa siku moja usiku, na alikuwa mmoja wao, akauliza,

51“Je, sheria zetu zinaturuhusu kumhukumu mtu kabla ya kumsikiliza na kufahamu alilotenda?”

52Wakamjibu, “Je, wewe pia unatoka Galilaya? Chunguza nawe utaona kwamba hakuna nabii atokae Galilaya!”

[

53Kisha wakaondoka, kila mtu akarudi nyumbani mwake.

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help