1Katika mwaka wa nne wa utawala wa Mfalme Dario, neno la Mwenyezi Mungu lilimjia Zekaria siku ya nne ya mwezi wa tisa, mwezi wa Kisleu.
2Watu wa Betheli walikuwa wamemtuma Shareza na Regem-Meleki pamoja na watu wao, kumsihi Mwenyezi Mungu
3kwa kuwauliza makuhani wa nyumba ya Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni na manabii, “Je, imempasa kuomboleza na kufunga katika mwezi wa tano, kama ambavyo nimekuwa nikifanya kwa miaka mingi?”
4Kisha neno la Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni likanijia kusema:
5“Waulize watu wote wa nchi na makuhani, ‘Je, mlipofunga na kuomboleza katika mwezi wa tano na wa saba kwa miaka sabini iliyopita, mlifunga kweli kwa ajili yangu?
6Na mlipokuwa mkila na kunywa, je, hamkuwa mnasherehekea kwa ajili ya nafsi zenu?
7Je, haya sio maneno ya Mwenyezi Mungu aliyosema kupitia manabii waliotangulia, wakati Yerusalemu pamoja na miji inayoizunguka ilipokuwa katika hali ya utulivu na ya mafanikio, wakati Negebu na Shefela zikiwa zimekaliwa na watu?’ ”
8Neno la Mwenyezi Mungu likamjia tena Zekaria:
9“Hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni: ‘Fanyeni hukumu za haki, onesheni rehema na huruma ninyi kwa ninyi.
10Msimdhulumu mjane wala yatima, mgeni wala maskini. Msiwaziane mabaya mioyoni mwenu ninyi kwa ninyi.’
11“Lakini wakakataa kusikiliza, wakanipa kisogo kwa ukaidi na kuziba masikio yao.
12Wakaifanya mioyo yao migumu kama gumegume, na hawakuisikiliza sheria au maneno ambayo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni aliyatuma kwa Roho wake Mtakatifu kupitia manabii waliotangulia. Kwa hiyo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, alikasirika sana.
13“ ‘Nilipoita, hawakusikiliza; kwa hiyo walipoita, sikusikiliza,’ asema Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni.
14‘Niliwatawanya kwa upepo wa kisulisuli miongoni mwa mataifa yote, mahali ambapo walikuwa wageni. Nchi ikaachwa ukiwa nyuma yao kiasi kwamba hakuna aliyeweza kuingia au kutoka. Hivi ndivyo walivyoifanya ile nchi iliyokuwa imependeza kuwa ukiwa.’ ”
Who We AreWhat We EelieveWhat We Do
2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.