Yoshua Utangulizi - Kiswahili Contemporary Scriptures 2024
UtanguliziKitabu hiki kinachukua jina la mhusika wake mkuu, yaani Yoshua mwana wa Nuni, ambaye alitoka kwenye kabila la Efraimu (Hesabu 13:8). Yoshua maana yake ni “Yehova (Mwenyezi Mungu) ni wokovu”; Yoshua alichaguliwa na Mwenyezi Mungu kuwa kiongozi muda mfupi kabla ya kifo cha Musa (Kumbukumbu 31). Maandalizi kwa ajili ya huduma yake yanajumuisha: Kiongozi wa jeshi la Israeli kupigana na Waamaleki (Kutoka 17:8-16); msaidizi wa Musa (Kutoka 33:11); mmoja wa wale wapelelezi 12 walioenda kupeleleza Kanaani (Hesabu 13–14); kuchaguliwa kwake kuchukua nafasi ya Musa kwa sababu ya upekee wa huduma yake (Hesabu 27:18-23; Kumbukumbu 1:38; 31:7-8).Ingawa makabila ya Reubeni na Gadi, na nusu ya kabila la Manase, tayari walikwisha miliki eneo la mashariki mwa Mto Yordani chini ya uongozi wa Musa, makabila yaliyosalia yalipata sehemu zao chini ya uongozi wa Yoshua. Kabila la Lawi halikupewa mgawo wa urithi katika nchi, bali walipewa miji 48 kuwa miliki yao katika nchi nzima, ili waweze kutoa huduma yao ya kiroho kwa sababu walipewa ukuhani.Kabla Yoshua hajafariki, aliwakumbusha watu kuhusu agano la Mwenyezi Mungu na ahadi zake kwao, na akawaonya kuhusu kuabudu sanamu. Yeye aliweka wazi upya agano kati ya Mwenyezi Mungu na Israeli, akiwaonya Waisraeli kudumisha ile hali ya kujitoa kwa Mwenyezi Mungu na kumpenda kwa moyo wote. Aliwaelekeza watu waendelee kumpenda, kumtii na kumtumikia Mwenyezi Mungu. Alizungumza hadharani jinsi yeye binafsi alivyokuwa tayari kumtumikia Mwenyezi Mungu aliposema, “Chagueni hivi leo mtakayemtumikia, lakini mimi na nyumba yangu tutamtumikia Mwenyezi Mungu” (24:15).MwandishiYoshua, isipokuwa sehemu ya mwisho ambayo inasemekana iliandikwa na Finehasi, kuhani mkuu.KusudiKitabu cha Yoshua kinaeleza historia ya Waisraeli na jinsi walivyotwaa Nchi ya Ahadi kwa ushindi.MahaliKanaani, iliyokuwa Nchi ya Ahadi.TareheKama mwaka wa 1370 K.K.Wahusika WakuuYoshua, Rahabu, Akani, Finehasi, na Eleazari.Wazo KuuKitabu hiki kinashughulika na ukamilisho wa ahadi ya kuimiliki nchi ya Kanaani.Mambo MuhimuKuvuka Mto Yordani (3:1-17), kusimamisha kumbukumbu ya mawe (4:1-9), tohara, kuadhimisha Pasaka (5:10), na kuuteka mji wa Yeriko (6:1-27).YaliyomoMaandalizi ya kuiteka Kanaani (1:1–5:15)Kuishinda Kanaani (6:1–12:24)Mgawanyo wa nchi kwa makabila (13:1–21:45)Kuagana na Yoshua, na kifo chake (22:1–24:33).