1 Wafalme 19 - Kiswahili Contemporary Scriptures 2024

Ilya akimbilia Horebu

1Ahabu akamwambia Yezebeli kila kitu Ilya alichokuwa amefanya na jinsi alivyowaua manabii wote kwa upanga.

2Hivyo Yezebeli akamtuma mjumbe kwa Ilya, kusema, “Miungu waniadhibu vikali zaidi, ikiwa kesho wakati kama huu sitakuwa nimeondoa uhai wako kama mmoja wa hao manabii.”

3Ilya aliogopa, na akatoroka kuokoa maisha yake. Alipofika Beer-Sheba katika Yuda, akamwacha mtumishi wake huko,

4lakini yeye mwenyewe akatembea mwendo wa kutwa nzima katika jangwa. Akafika kwenye mti wa mretemu, akakaa chini yake na kuomba ili afe. Akasema, “Yatosha sasa, Mwenyezi Mungu, ondoa roho yangu, kwani mimi si bora kuliko baba zangu.”

5Kisha akajinyoosha chini ya mti, akalala usingizi.

Mara malaika akamgusa na kumwambia, “Inuka ule.”

6Akatazama pande zote, na hapo karibu na kichwa chake palikuwa na mkate uliookwa kwenye makaa ya moto, na gudulia la maji. Akala na kunywa, kisha akajinyoosha tena.

7Yule malaika wa Mwenyezi Mungu akaja tena mara ya pili, akamgusa na kumwambia, “Inuka ule, kwa kuwa bado una safari ndefu mbele yako.”

8Kwa hiyo akainuka, akala na kunywa. Akiwa ametiwa nguvu na kile chakula, akasafiri siku arobaini usiku na mchana hadi akafika Horebu, mlima wa Mungu.

9Huko akaingia katika pango, akalala humo usiku ule.

Mwenyezi Mungu amtokea Ilya

Nalo neno la Mwenyezi Mungu likamjia, kusema, “Unafanya nini hapa, Ilya?”

10Akajibu, “Nimekuwa nikifanya bidii sana kwa ajili ya Bwana Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni. Waisraeli wamelikataa agano lako, wamevunja madhabahu zako na kuwaua manabii wako kwa upanga. Ni mimi peke yangu niliyebaki, sasa wananitafuta ili waniue pia.”

11Mwenyezi Mungu akasema, “Toka nje ukasimame juu ya mlima mbele za Mwenyezi Mungu, kwa kuwa Mwenyezi Mungu yu karibu kupita hapo.”

Kisha upepo mzito na wenye nguvu ukapasua milima ile na kuvunjavunja miamba mbele za Mwenyezi Mungu, lakini Mwenyezi Mungu hakuwamo katika ule upepo. Baada ya upepo palikuwa na tetemeko la ardhi, lakini Mwenyezi Mungu hakuwamo kwenye lile tetemeko.

12Baada ya tetemeko la ardhi moto ukaja, lakini Mwenyezi Mungu hakuwamo katika ule moto. Baada ya moto ikaja sauti ya utulivu ya kunong’ona.

13Ilya alipoisikia, akafunika uso kwa vazi lake, akatoka na kusimama kwenye mlango wa pango.

Kisha ile sauti ikamwambia, “Ilya, unafanya nini hapa?”

14Akajibu, “Nimekuwa nikifanya bidii sana kwa ajili ya Bwana Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni. Waisraeli wamelikataa agano lako, wamevunja madhabahu zako na kuwaua manabii wako kwa upanga. Ni mimi peke yangu niliyebaki, sasa wananitafuta ili waniue pia.”

15Mwenyezi Mungu akamwambia, “Rudi kwa njia uliyoijia, uende kwenye Jangwa la Dameski. Utakapofika huko, mpake Hazaeli mafuta awe mfalme wa Aramu.

16Pia mpake mafuta Yehu, mwana wa Nimshi awe mfalme wa Israeli, na umpake mafuta Al-Yasa mwana wa Shafati kutoka Abel-Mehola awe nabii baada yako.

17Yehu atamuua yeyote atakayeutoroka upanga wa Hazaeli, naye Al-Yasa atamuua yeyote atakayeutoroka upanga wa Yehu.

18Hata sasa nimeweka akiba ya watu elfu saba katika Israeli, wote ambao hawajampigia Baali magoti, na wote ambao midomo yao haijambusu.”

Wito wa Al-Yasa

19Hivyo Ilya akaondoka huko na kumkuta Al-Yasa mwana wa Shafati. Alikuwa akilima kwa jozi kumi na mbili za maksai, na yeye mwenyewe aliiongoza ile jozi ya kumi na mbili. Ilya akamwendea, na kumvisha vazi lake.

20Kisha Al-Yasa akawaacha maksai wake, akamkimbilia Ilya, akamwambia, “Niruhusu nikawabusu baba yangu na mama yangu, halafu nitafuatana nawe.”

Ilya akajibu, “Rudi zako, kwani nimekufanya nini?”

21Basi Al-Yasa akamwacha Ilya, naye akarudi. Akachukua ile jozi yake ya maksai na kuwachinja. Akaipika ile nyama kwa kutumia miti ya nira kama kuni na kuwapa watu, nao wakala. Kisha akaondoka, akamfuata Ilya, akamtumikia.

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help