1Heri mtu yule anayemjali mnyonge,
Mwenyezi Mungu atamwokoa wakati wa shida.
2Mwenyezi Mungu atamlinda na kuyahifadhi maisha yake,
atambariki katika nchi
na hatamwacha katika tamaa ya adui zake.
3Mwenyezi Mungu atamtegemeza akiwa mgonjwa kitandani,
na atamwinua kutoka kitandani mwake.
4Nilisema, “Ee Mwenyezi Mungu nihurumie,
niponye, maana nimekutenda dhambi wewe.”
5Adui zangu wanasema kwa hila,
“Lini atakufa, na jina lake litokomee kabisa.”
6Kila anapokuja mtu kunitazama,
huzungumza uongo,
huku moyo wake ukikusanya masingizio;
kisha huondoka na kuyasambaza.
7Adui zangu wote hunong’onezana dhidi yangu,
hao huniwazia mabaya sana, wakisema,
8“Ugonjwa mbaya sana umempata,
kamwe hatainuka tena kitandani mwake.”
9Hata rafiki yangu wa karibu niliyemwamini,
yule aliyekula chakula changu
ameniinulia kisigino chake.
10Lakini wewe, Ee Mwenyezi Mungu, nihurumie,
ukaniinue tena, ili niweze kuwalipiza kisasi.
11Najua kwamba wapendezwa nami,
kwa kuwa adui yangu hanishindi.
12Katika uadilifu wangu unanitegemeza
na kuniweka kwenye uwepo wako milele.
13Mtukuzeni Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli,
tangu milele na hata milele.
Amen na Amen.
Who We AreWhat We EelieveWhat We Do
2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.