Danieli 12 - Kiswahili Contemporary Scriptures 2024

Nyakati za mwisho

1“Katika wakati huo Mikaeli, mtawala mkuu ambaye huwalinda watu wako, atainuka. Kutakuwako wakati wa taabu ambao haujatokea tangu mwanzo wa mataifa hadi wakati huo. Lakini wakati huo, watu wako, kila mmoja ambaye jina lake litakutwa limeandikwa kwenye kitabu, ataokolewa.

2Wengi ambao wamelala kwenye mavumbi wataamka, baadhi yao kwa uzima wa milele, wengine kwa aibu na kudharauliwa milele.

3Wale wenye hekima watang’aa kama mwanga wa mbingu, nao wale ambao huwaongoza wengi kutenda haki, watang’aa kama nyota milele na milele.

4Lakini wewe Danieli, yafunge na kuyatia muhuri maneno ya kitabu hiki hadi wakati wa mwisho. Wengi wataenda hapa na pale, na maarifa yataongezeka.”

5Ndipo mimi Danieli nikaangalia, nako mbele yangu walisimama wengine wawili, mmoja katika ukingo huu wa mto, na mwingine ukingo wa pili wa mto.

6Mmoja wao akamwambia yule mtu aliyevaa nguo za kitani, aliyekuwa juu ya maji ya mto, “Je, itachukua muda gani kabla mambo haya ya kushangaza hayajatimizwa?”

7Kisha mtu yule aliyevaa nguo za kitani, aliyekuwa juu ya maji ya mto, akainua mkono wake wa kuume na mkono wake wa kushoto kuelekea mbinguni, nami nikamsikia akiapa kwa jina lake yeye aishiye milele, akisema, “Itakuwa wakati, nyakati mbili, na nusu wakati. Nguvu za watu watakatifu zitakapokuwa zimevunjwa kabisa, ndipo mambo haya yote yatakapotimizwa.”

8Nilisikia, lakini sikuelewa. Kwa hiyo nikauliza, “Bwana wangu, matokeo ya haya yote yatakuwa nini?”

9Akajibu, “Danieli, nenda zako, kwa sababu maneno haya yamefungwa na kutiwa muhuri hadi wakati wa mwisho.

10Wengi watatakaswa, na kuondolewa mawaa na kufanywa safi, lakini waovu wataendelea kuwa waovu. Hakuna mmoja wa waovu atakayefahamu, lakini wale wenye hekima watafahamu.

11“Tangu wakati ule wa kukomeshwa kwa dhabihu ya kila siku, na kuanzishwa kwa chukizo la uharibifu, kutakuwepo siku elfu moja na mia mbili na tisini (1,290).

12Kubarikiwa ni yule atakayevumilia hadi kufikia mwisho wa hizo siku elfu moja mia tatu na thelathini na tano (1,335).

13“Lakini wewe, nenda zako hadi mwisho. Utapumzika, nawe mwisho wa hizo siku utafufuka ili kuupokea urithi uliowekewa.”

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help