1Nitamtukuza Mwenyezi Mungu nyakati zote,
sifa zake zitakuwa mdomoni mwangu siku zote.
2Nafsi yangu itajisifu katika Mwenyezi Mungu,
walioonewa watasikia na wafurahi.
3Mtukuzeni Mwenyezi Mungu pamoja nami,
naam, na tulitukuze jina lake pamoja.
4Nilimtafuta Mwenyezi Mungu naye akanijibu,
akaniokoa kwenye hofu zangu zote.
5Wale wamtazamao hutiwa nuru,
nyuso zao hazifunikwi na aibu kamwe.
6Maskini huyu alimwita Mwenyezi Mungu, naye akamsikia,
akamwokoa katika taabu zake zote.
7Malaika wa Mwenyezi Mungu hufanya kituo
akiwazunguka wale wamchao,
naye huwaokoa.
8Onjeni mwone kwamba Mwenyezi Mungu ni mwema;
heri mtu yule anayemkimbilia.
9Mcheni Mwenyezi Mungu enyi watakatifu wake,
kwa maana wale wamchao
hawapungukiwi na chochote.
10Wana simba wenye nguvu
hutindikiwa na kuona njaa,
bali wale wanaomtafuta Mwenyezi Mungu
hawatakosa kitu chochote kilicho chema.
11Njooni, watoto wangu, mnisikilize,
nitawafundisha kumcha Mwenyezi Mungu.
12Yeyote kati yenu anayependa uzima
na kutamani kuziona siku nyingi njema,
13basi auzuie ulimi wake na mabaya,
na midomo yake kutokana na kusema uongo.
14Aache uovu, atende mema,
aitafute amani na kuifuatilia.
15Macho ya Mwenyezi Mungu huwaelekea wenye haki,
na masikio yake yako makini kusikiliza kilio chao.
16Uso wa Mwenyezi Mungu uko kinyume na watendao maovu,
ili kufuta kumbukumbu lao duniani.
17Wenye haki hulia, naye Mwenyezi Mungu huwasikia,
huwaokoa katika taabu zao zote.
18Mwenyezi Mungu yu karibu na waliovunjika moyo,
na huwaokoa waliopondeka roho.
19Mwenye haki ana mateso mengi,
lakini Mwenyezi Mungu humwokoa nayo yote,
20huhifadhi mifupa yake yote,
hata mmoja hautavunjika.
21Ubaya utamuua mtu mwovu,
nao adui za mwenye haki watahukumiwa.
22Mwenyezi Mungu huwakomboa watumishi wake,
yeyote anayemkimbilia yeye
hatahukumiwa kamwe.
Who We AreWhat We EelieveWhat We Do
2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.