Mithali 28 - Kiswahili Contemporary Scriptures 2024

1Mtu mwovu hukimbia ingawa hakuna yeyote anayemfukuza,

bali wenye haki ni wajasiri kama simba.

2Nchi inapokuwa na uasi,

inakuwa na viongozi wengi,

bali kiongozi mwenye ufahamu na maarifa

hudumisha utaratibu.

3Mtawala anayewadhulumu maskini,

ni kama mvua ya dhoruba inayoharibu mazao yote.

4Wale wanaoacha sheria huwasifu waovu,

bali wale wanaotii sheria huwapinga.

5Wapotovu hawaelewi haki,

bali wale wanaomtafuta Mwenyezi Mungu wanaielewa kikamilifu.

6Afadhali maskini ambaye mwenendo wake hauna lawama,

kuliko tajiri ambaye njia zake ni potovu.

7Yeye anayetii sheria ni mwana mwenye ufahamu,

bali rafiki wa walafi humwaibisha baba yake.

8Yeye aongezaye utajiri wake kwa riba kubwa mno

hukusanya kwa ajili ya mwingine,

ambaye atawahurumia maskini.

9Mtu yeyote akikataa kusikia sheria,

hata maombi yake ni chukizo.

10Yeye anayemwongoza mwenye haki kwenye mapito mabaya,

ataanguka kwenye mtego wake mwenyewe,

bali wasio na lawama watapokea urithi mwema.

11Mtu tajiri anaweza kuwa na hekima machoni pake mwenyewe,

bali mtu maskini mwenye busara

humtambua alivyodanganyika.

12Mwenye haki ashindapo, kuna furaha kubwa,

bali waovu watawalapo, watu hujificha.

13Yeye afichaye dhambi zake hatafanikiwa,

bali yeyote aziungamaye na kuziacha hupata rehema.

14Amebarikiwa mtu ambaye siku zote humcha Mwenyezi Mungu,

bali yeye afanyaye moyo wake kuwa mgumu

huanguka kwenye taabu.

15Kama simba angurumaye au dubu ashambuliaye,

ndivyo alivyo mtu mwovu anayetawala wanyonge.

16Mtawala dhalimu hana akili,

bali yeye achukiaye mapato ya udhalimu

atafurahia maisha marefu.

17Mtu mwenye kusumbuliwa na hatia ya kuua

atakuwa mtoro hadi kufa;

mtu yeyote asimsaidie.

18Yeye ambaye mwenendo wake hauna lawama

hulindwa salama,

bali yeye ambaye njia zake ni potovu

ataanguka ghafula.

19Yeye alimaye shamba lake atakuwa na chakula tele,

bali yule afuataye mambo ya upuzi atakuwa na umaskini wa kumtosha.

20Mtu mwaminifu atabarikiwa sana,

bali yeye atamaniye kupata utajiri kwa haraka

hataacha kuadhibiwa.

21Kuonesha upendeleo si vizuri,

hata hivyo mtu atafanya kosa kwa kipande cha mkate.

22Mtu mchoyo ana tamaa ya kupata utajiri,

naye hana habari kuwa umaskini unamngojea.

23Yeye amkemeaye mtu mwishoni hupata kibali zaidi,

kuliko mwenye maneno ya kusifu isivyostahili.

24Yeye amwibiaye babaye au mamaye

na kusema, “Si kosa,”

yeye ni mwenzi wa yule aharibuye.

25Mtu mwenye tamaa huchochea fitina,

bali yule amtegemeaye Mwenyezi Mungu atafanikiwa.

26Yeye ajitumainiaye mwenyewe ni mpumbavu,

bali yeye atembeaye katika hekima hulindwa salama.

27Yeye ampaye maskini

hatapungukiwa na kitu chochote,

bali yeye awafumbiaye maskini macho

hupata laana nyingi.

28Wakati waovu wanatawala,

watu huenda mafichoni,

bali waovu wanapoangamia,

wenye haki hufanikiwa.

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help