Waamuzi 13 - Kiswahili Contemporary Scriptures 2024

Kuzaliwa kwa Samsoni

1Waisraeli wakafanya maovu tena mbele za Mwenyezi Mungu. Hivyo Mwenyezi Mungu akawatia mikononi mwa Wafilisti kwa muda wa miaka arobaini.

2Palikuwa na mtu mmoja wa Sora, aliyeitwa Manoa, wa ukoo wa Wadani, naye alikuwa na mke aliyekuwa tasa, asiyeweza kuzaa watoto.

3Malaika wa Mwenyezi Mungu akamtokea huyo mwanamke na kumwambia, “Wewe ni tasa na huna mtoto, lakini utachukua mimba na utamzaa mtoto wa kiume.

4Lakini ujihadhari sana usinywe divai wala kileo kingine chochote, wala usile kitu chochote kilicho najisi,

5kwa kuwa utachukua mimba na utamzaa mtoto wa kiume. Wembe usipite kwenye kichwa chake, kwa kuwa huyo mwana atakuwa Mnadhiri aliyetengwa kwa Mungu tangu tumboni mwa mama yake. Naye atawaongoza na kuwaokoa Waisraeli kutoka mikononi mwa Wafilisti.”

6Ndipo huyo mwanamke akamwendea mumewe na kumwambia, “Mtu wa Mungu alinijia. Alionekana kama malaika wa Mungu, wa kutisha sana. Sikumuuliza alikotoka wala hakuniambia jina lake.

7Lakini aliniambia, ‘Utachukua mimba na utazaa mtoto wa kiume. Basi sasa, usinywe divai wala kileo kingine chochote, wala usile kitu kilicho najisi, kwa kuwa huyo mtoto atakuwa Mnadhiri wa Mungu tangu tumboni mwa mama yake hadi kufa kwake.’ ”

8Ndipo Manoa akamwomba Mwenyezi Mungu, akasema: “Ee Bwana, nakusihi huyo mtu wa Mungu uliyemtuma kwetu aje tena, ili atufundishe jinsi ya kumlea huyo mwana atakayezaliwa.”

9Mungu akamsikia Manoa, naye malaika wa Mungu akamjia tena huyo mwanamke alipokuwa shambani; lakini mumewe Manoa hakuwa naye.

10Basi yule mwanamke akaenda haraka na kumwambia mumewe, “Tazama mtu yule aliyenitokea siku ile yupo hapa!”

11Manoa akainuka akaandamana na mkewe. Alipomfikia yule mtu akamuuliza, “Je, wewe ndiwe ulisema na mke wangu?”

Akasema, “Ni mimi.”

12Basi Manoa akamuuliza, “Maneno yako yatakapotimia, je, masharti ya maisha ya mtoto huyu yatakuwa ni yapi, na kazi yake itakuwa ni ipi?”

13Malaika wa Mwenyezi Mungu akamjibu, “Mke wako hana budi kufanya yale yote niliyomwambia.

14Kamwe asile kitu chochote kitakachotoka katika mzabibu, wala asinywe divai yoyote wala kileo chochote, wala asile kitu chochote kilicho najisi. Hana budi kufanya kila kitu nilichomwagiza.”

15Manoa akamjibu yule malaika wa Mwenyezi Mungu, “Twakuomba usubiri kwanza ili tuweze kuandaa mwana-mbuzi kwa ajili yako.”

16Malaika wa Mwenyezi Mungu akamjibu, “Hata kama utanizuia, sitakula chochote kwako. Lakini ukitaka kuandaa sadaka ya kuteketezwa, mtolee Mwenyezi Mungu.”

(Manoa hakumtambua kuwa huyu alikuwa malaika wa Mwenyezi Mungu.)

17Kisha Manoa akamuuliza yule malaika wa Mwenyezi Mungu, “Jina lako ni nani, ili tuweze kukupa heshima wakati maneno uliyonena yatakapotimia?”

18Malaika wa Mwenyezi Mungu akamjibu, “Kwa nini unauliza jina langu? Ni jina la ajabu.”

19Ndipo Manoa akamchukua mwana-mbuzi, pamoja na sadaka ya unga, naye akamtolea Mwenyezi Mungu dhabihu hapo juu ya mwamba. Naye yule malaika wa Mwenyezi Mungu akafanya jambo la ajabu wakati Manoa na mkewe wakiwa wanaangalia:

20Mwali wa moto kutoka hapo madhabahuni ulipowaka kuelekea mbinguni, malaika wa Mwenyezi Mungu akapaa ndani ya huo mwali. Manoa na mkewe, kwa kuona jambo hili, wakaanguka kifudifudi.

21Malaika wa Mwenyezi Mungu hakumtokea tena Manoa na mkewe. Ndipo Manoa akatambua kuwa huyo alikuwa malaika wa Mwenyezi Mungu.

22Manoa akamwambia mkewe, “Hakika tutakufa, kwa kuwa tumemwona Mungu.”

23Lakini mkewe akamwambia, “Ikiwa Mwenyezi Mungu alikuwa amekusudia kutuua, hangepokea sadaka ya kuteketezwa na sadaka ya unga kutoka mikononi mwetu, wala hangetuonesha mambo haya yote wala kututangazia mambo haya wakati huu.”

24Yule mwanamke akazaa mtoto wa kiume, akamwita jina Samsoni. Kijana akakua, naye Mwenyezi Mungu akambariki.

25Roho wa Mwenyezi Mungu akaanza kumpa msukumo alipokuwa huko Mahane-Dani, kati ya Sora na Eshtaoli.

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help