1Yehoshafati mwanawe akawa mfalme baada yake na akajiimarisha dhidi ya Israeli.
2Akaweka jeshi katika miji yote ya Yuda yenye ngome, na kuweka askari walinzi katika Yuda na katika miji ya Efraimu ambayo baba yake Asa alikuwa ameiteka.
3Mwenyezi Mungu alikuwa na Yehoshafati kwa sababu katika miaka yake ya mwanzoni alienenda katika njia za Daudi baba yake. Hakutafuta Mabaali
4bali alimtafuta Mungu wa baba yake na kuzifuata amri zake badala ya kufuata desturi za Waisraeli.
5Kwa hiyo Mwenyezi Mungu akauimarisha ufalme chini ya uongozi wake, nao Yuda wote wakamletea Yehoshafati zawadi, hivyo akawa na utajiri mwingi na heshima.
6Moyo wake ukawa hodari katika njia za Mwenyezi Mungu na zaidi ya yote, akaondoa mahali pa juu pa kuabudia na nguzo za Maashera katika Yuda.
7Katika mwaka wa tatu wa utawala wake Yehoshafati, alituma maafisa wake ambao ni Ben-Haili, Obadia, Zekaria, Nethaneli na Mikaya ili kufundisha katika miji ya Yuda.
8Pamoja nao walikuwa na Walawi kadhaa: Shemaya, Nethania, Zebadia, Asaheli, Shemiramothi, Yehonathani, Adoniya, Tobia, Tob-Adonia; na pamoja nao makuhani Elishama na Yehoramu.
9Wakafundisha Yuda yote, wakiwa wamechukua Kitabu cha Torati ya Mwenyezi Mungu; wakazunguka miji yote ya Yuda na kufundisha watu.
10Kicho cha Mwenyezi Mungu kikawa juu ya falme zote za nchi zilizozunguka Yuda, hivyo hawakufanya vita na Yehoshafati.
11Baadhi ya Wafilisti wakamletea Yehoshafati zawadi na fedha kama ushuru, nao Waarabu wakamletea mifugo: kondoo dume elfu saba na mia saba, na mbuzi elfu saba na mia saba.
12Yehoshafati akaendelea kupata nguvu zaidi na zaidi, akajenga ngome na miji ya hazina katika Yuda,
13na akawa na vifaa vingi katika miji ya Yuda. Pia aliweka wapiganaji wenye uzoefu huko Yerusalemu.
14Wakaandikishwa katika jamaa zao kama ifuatavyo:
Kutoka Yuda, majemadari wa vikosi vya elfu:
Jemadari Adna akiwa na wapiganaji elfu mia tatu;
15aliyefuata ni jemadari Yehohanani, akiwa na wapiganaji elfu mia mbili na themanini;
16aliyefuata ni Amasia mwana wa Zikri, ambaye alijitolea kwa ajili ya kazi ya Mwenyezi Mungu, akiwa na wapiganaji elfu mia mbili.
17Kutoka Benyamini:
Eliada, mpiganaji hodari, akiwa na watu elfu mia mbili wenye nyuta na ngao;
18aliyefuata ni Yehozabadi, akiwa na wapiganaji elfu mia moja na themanini tayari kwa vita.
19Hawa ndio wapiganaji waliomtumikia mfalme, mbali na ambao mfalme aliwaweka katika miji yenye ngome katika Yuda yote.
Who We AreWhat We EelieveWhat We Do
2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.