Isaya 64 - Kiswahili Contemporary Scriptures 2024

1Laiti ungepasua mbingu na kushuka chini,

ili milima itetemeke mbele zako!

2Kama vile moto unavyoteketeza vijiti

na kusababisha maji kuchemka,

shuka ukafanye jina lako lijulikane kwa adui zako,

na kusababisha mataifa yatetemeke mbele zako!

3Kwa maana ulipofanya mambo ya kutisha ambayo hatukuyatazamia,

ulishuka, nayo milima ikatetemeka mbele zako.

4Tangu nyakati za zamani hakuna yeyote aliyesikia,

hakuna sikio lililotambua,

hakuna jicho lililomwona Mungu mwingine ila wewe,

anayetenda mambo kwa ajili ya wale wamngojeao.

5Uliwasaidia watu wale watendao yaliyo haki kwa furaha,

wale wazikumbukao njia zako.

Lakini wakati tulipoendelea kutenda dhambi kinyume na njia zako,

ulikasirika.

Tutawezaje basi kuokolewa?

6Sisi sote tumekuwa kama mtu aliye najisi,

nayo matendo yetu yote ya uadilifu ni kama matambaa machafu;

sisi sote tunasinyaa kama jani,

na kama upepo maovu yetu hutupeperusha.

7Hakuna yeyote anayeliitia jina lako

wala anayejitahidi kukushika,

kwa kuwa umetuficha uso wako

na kutuacha tudhoofike kwa sababu ya dhambi zetu.

8Lakini, Ee Mwenyezi Mungu, wewe ndiwe Baba yetu.

Sisi ni udongo, na wewe ndiwe mfinyanzi;

sisi sote tu kazi ya mkono wako.

9Ee Mwenyezi Mungu, usikasirike kupita kiasi,

usizikumbuke dhambi zetu milele.

Ee Bwana, utuangalie, twakuomba,

kwa kuwa sisi sote tu watu wako.

10Miji yako mitakatifu imekuwa jangwa;

hata Sayuni ni jangwa, Yerusalemu ni ukiwa.

11Hekalu letu takatifu na tukufu,

ambako baba zetu walikusifu wewe,

limechomwa kwa moto,

navyo vitu vyote tulivyovithamini

vimeharibika.

12Ee Mwenyezi Mungu, baada ya haya yote, utajizuia?

Je, utanyamaza, na kutuadhibu kupita kiasi?

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help