Zaburi 64 - Kiswahili Contemporary Scriptures 2024

Zaburi 64Kuomba ulinzi dhidi ya aduiKwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi.

1Ee Mungu, unisikie ninapoeleza lalamiko langu,

uyahifadhi maisha yangu kutokana na vitisho vya adui.

2Unifiche kutokana na njama za waovu,

kutokana na fitina za kundi la watenda maovu.

3Wananoa ndimi zao kama panga

na kuelekeza maneno yao kama mishale ya kufisha.

4Hurusha mishale kutoka mavizio kwa mtu asiye na hatia,

humrushia ghafula bila woga.

5Kila mmoja humtia moyo mwenzake

katika mipango mibaya;

huzungumza kuhusu kuficha mitego yao,

nao husema, “Ni nani ataiona?”

6Hupanga njama la dhuluma na kusema,

“Tumebuni mpango mkamilifu!”

Hakika nia na moyo wa mwanadamu vina hila.

7Bali Mungu atawapiga kwa mishale,

nao ghafula wataangushwa.

8Atageuza ndimi zao wenyewe dhidi yao

na kuwaleta kwenye maangamizi;

wote wawaonao watatikisa vichwa vyao

kwa dharau.

9Wanadamu wote wataogopa,

watatangaza kazi za Mungu

na kutafakari yale aliyoyatenda.

10Wenye haki na wafurahi katika Mwenyezi Mungu,

na wakimbilie kwake;

wanyofu wote wa moyo na wamsifu yeye!

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help