Zaburi 147 - Kiswahili Contemporary Scriptures 2024

Zaburi 147Kumsifu Mwenyezi Mungu

1Msifuni Mwenyezi Mungu.

Tazama jinsi ilivyo vyema kumwimbia Mungu wetu sifa,

jinsi inavyopendeza na kustahili kumsifu yeye!

2Mwenyezi Mungu hujenga Yerusalemu,

huwakusanya Israeli walio uhamishoni.

3Anawaponya waliovunjika mioyo

na kuvifunga vidonda vyao.

4Huzihesabu nyota

na huipa kila moja jina lake.

5Bwana wetu ni mkuu na mwenye uwezo mwingi,

ufahamu wake hauna kikomo.

6Mwenyezi Mungu huwahifadhi wanyenyekevu

lakini huwashusha waovu hadi mavumbini.

7Mwimbieni Mwenyezi Mungu kwa shukrani,

mpigieni Mungu wetu kinubi.

8Yeye huzifunika anga kwa mawingu,

huinyeshea ardhi mvua,

na kuzifanya nyasi kuota juu ya vilima.

9Huwapa chakula mifugo

na pia makinda ya kunguru yanapolia.

10Furaha yake haipo katika nguvu za farasi,

wala furaha yake kwenye miguu ya shujaa.

11Mwenyezi Mungu hupendezwa na wale wamchao,

wale wanaoweka tumaini lao katika upendo wake usiokoma.

12Mtukuze Mwenyezi Mungu, ee Yerusalemu,

msifu Mungu wako, ee Sayuni,

13kwa maana huimarisha makomeo ya malango yako

na huwabariki watu wako walio ndani yako.

14Huwapa amani mipakani mwenu

na kukushibisha kwa ngano safi kabisa.

15Hutuma amri yake duniani,

neno lake hukimbia kasi.

16Anatandaza theluji kama sufu

na kutawanya umande kama majivu.

17Huvurumisha mvua yake ya mawe kama changarawe.

Ni nani awezaye kustahimili ukali wa baridi yake?

18Hutuma neno lake na kuviyeyusha,

huvumisha upepo wake, nayo maji hutiririka.

19Amemfunulia Yakobo neno lake,

sheria zake na maagizo yake kwa Israeli.

20Hajafanya hivyo kwa taifa lingine lolote,

hawazijui sheria zake.

Msifuni Mwenyezi Mungu.

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help