1“Ole wao wachungaji wanaoharibu na kutawanya kondoo wa malisho yangu!” asema Mwenyezi Mungu.
2Kwa hiyo hili ndilo Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, analowaambia wachungaji wanaowachunga watu wangu: “Kwa sababu mmelitawanya kundi langu na kuwafukuzia mbali, wala hamkuwatunza, basi mimi nitawaadhibu kwa ajili ya uovu mliofanya,” asema Mwenyezi Mungu.
3“Mimi mwenyewe nitayakusanya mabaki ya kundi langu kutoka nchi zote ambazo nimewafukuzia, nami nitawarudisha katika malisho yao, ambapo watazaa na kuongezeka idadi yao.
4Nitaweka wachungaji juu yao ambao watawachunga, nao hawataogopa tena au kutishwa, wala hatapotea hata mmoja,” asema Mwenyezi Mungu.
5Mwenyezi Mungu asema, “Siku zinakuja,
nitakapomwinulia Daudi Tawi lenye haki,
Mfalme atakayetawala kwa hekima,
na kutenda lililo haki na sawa katika nchi.
6Katika utawala wake, Yuda ataokolewa,
na Israeli ataishi salama.
Hili ndilo jina atakaloitwa:
Mwenyezi Mungu ni Haki Yetu.”
7Mwenyezi Mungu asema, “Hivyo basi, siku zinakuja, ambapo watu hawatasema tena, ‘Hakika kama Mwenyezi Mungu aishivyo, aliyewapandisha Waisraeli kutoka Misri,’
8bali watasema, ‘Hakika kama Mwenyezi Mungu aishivyo, aliyewatoa wazao wa Israeli kutoka nchi ya kaskazini na nchi zote alizokuwa amewafukuzia.’ Ndipo wataishi katika nchi yao wenyewe.”
Manabii wasemao uongo9Kuhusu manabii:
Moyo wangu umevunjika ndani yangu;
mifupa yangu yote inatetemeka.
Nimekuwa kama mtu aliyelewa,
kama mtu aliyelemewa na divai,
kwa sababu ya Mwenyezi Mungu
na maneno yake matakatifu.
10Nchi imejaa wazinzi;
kwa sababu ya laana, nchi imekauka,
na malisho ya nyikani yamekauka.
Mwenendo wa manabii ni mbaya
na mamlaka yao si ya haki.
11“Nabii na kuhani wote si wacha Mungu;
hata hekaluni mwangu ninaona uovu wao,”
asema Mwenyezi Mungu.
12“Kwa hiyo mapito yao yatakuwa utelezi,
watafukuziwa mbali gizani
na huko wataanguka.
Nitaleta maafa juu yao
katika mwaka wa kuadhibiwa kwao,”
asema Mwenyezi Mungu.
13“Miongoni mwa manabii wa Samaria
nililiona jambo la kuchukiza:
Walitabiri kwa Baali
na kuwapotosha Israeli watu wangu.
14Nako miongoni mwa manabii wa Yerusalemu
nimeona jambo baya sana:
Wanafanya uzinzi
na kuenenda katika uongo.
Wanatia nguvu mikono ya watenda maovu,
kwa ajili hiyo hakuna yeyote
anayeachana na uovu wake.
Wote wako kama Sodoma kwangu;
watu na Yerusalemu wako kama Gomora.”
15Kwa hiyo, hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni kuhusu manabii:
“Nitawafanya wale chakula kichungu
na kunywa maji yaliyotiwa sumu,
kwa sababu kutokana na manabii wa Yerusalemu
kutokumcha Mungu kumeenea katika nchi yote.”
16Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni:
“Msisikilize wanachowatabiria manabii,
wanawajaza matumaini ya uongo.
Wanasema maono kutoka akili zao wenyewe,
hayatoki katika kinywa cha Mwenyezi Mungu.
17Huendelea kuwaambia wale wanaonidharau mimi,
‘Mwenyezi Mungu asema: Mtakuwa na amani.’
Kwa wale wote wafuatao ugumu wa mioyo yao,
wao husema, ‘Hakuna dhara litakalowapata.’
18Lakini ni yupi miongoni mwao aliyesimama katika baraza la Mwenyezi Mungu
ili kuona au kusikia neno lake?
Ni nani aliyesikiliza
na kusikia neno lake?
19Tazama, dhoruba ya Mwenyezi Mungu
itatokea kwa ghadhabu,
kisulisuli kitazunguka na kuanguka
juu ya vichwa vya waovu.
20Hasira ya Mwenyezi Mungu haitageuka
hadi amelitimiza kusudi la moyo wake.
Siku zijazo mtalifahamu kwa wazi.
21Mimi sikuwatuma manabii hawa,
lakini bado wamekimbia wakitangaza ujumbe wao.
Mimi sikusema nao,
lakini wametabiri.
22Lakini kama wangesimama barazani pangu,
wangetangaza maneno yangu kwa watu wangu,
nao wangewageuza kutoka njia zao mbaya
na kutoka matendo yao maovu.
23“Je, mimi ni Mungu aliye karibu tu,
wala si Mungu aliye pia mbali?”
Mwenyezi Mungu asema.
24“Je, mtu yeyote aweza kujificha
mahali pa siri nisiweze kumwona?”
Mwenyezi Mungu asema.
“Je, mimi sikuijaza mbingu na nchi?”
Mwenyezi Mungu asema.
25“Nimesikia wanayoyasema manabii, hao wanaotabiri uongo kwa jina langu. Wanasema, ‘Nimeota ndoto! Nimeota ndoto!’
26Mambo haya yataendelea hata lini ndani ya mioyo ya hawa manabii wa uongo, ambao hutabiri maono ya uongo ya akili zao wenyewe?
27Wanadhani ndoto wanazoambiana wao kwa wao zitawafanya watu wangu walisahau jina langu, kama baba zao walivyolisahau kwa kumwabudu Baali.
28Mwache nabii aliye na ndoto aseme ndoto yake, lakini yule aliye na neno langu na aliseme kwa uaminifu. Kwa maana jani kavu lina uhusiano gani na ngano?” asema Mwenyezi Mungu.
29“Je, neno langu si kama moto,” asema Mwenyezi Mungu, “na kama nyundo ivunjayo mwamba vipande vipande?
30“Kwa hiyo, niko kinyume na manabii wanaoibiana maneno kana kwamba ni yangu,” asema Mwenyezi Mungu.
31“Naam, mimi niko kinyume na manabii wanaotumia ndimi zao wenyewe na kusema, ‘Mwenyezi Mungu asema.’
32Kweli, niko kinyume na hao wanaotabiri ndoto za uongo,” asema Mwenyezi Mungu. “Wanazisimulia na kuwapotosha watu wangu kwa uongo wao bila kujali, lakini sikuwatuma wala sikuwaamuru. Hawawafaidi watu hawa hata kidogo,” asema Mwenyezi Mungu.
Unabii wa uongo33“Basi watu hawa, au nabii, au kuhani, watakapokuuliza, ‘Ujumbe wa Mwenyezi Mungu ni nini?’ Wewe utawaambia, ‘Ninyi ndio ujumbe. Nami nitawavua kama vazi, asema Mwenyezi Mungu.’
34Nabii, kuhani, au mtu yeyote akisema, ‘Huu ndio ujumbe wa Mwenyezi Mungu,’ nitamwadhibu huyo na nyumba yake.
35Mnaambiana kila mmoja na mwenzake, au kwa mtu wa nyumba yao: ‘Mwenyezi Mungu amejibu nini?’ au ‘Mwenyezi Mungu amesema nini?’
36Lakini kamwe msiseme tena, ‘Nina ujumbe wa Mwenyezi Mungu,’ kwa sababu kila neno la mtu binafsi linakuwa mzigo wake mwenyewe, na hivyo kupotosha maneno ya Mungu aliye hai, Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, Mungu wetu.
37Hivi ndivyo utakavyoendelea kumuuliza nabii: ‘Mwenyezi Mungu amekujibu nini?’ au ‘Je, Mwenyezi Mungu amesema nini?’
38Ingawa unadai, ‘Huu ndio ujumbe wa Mwenyezi Mungu,’ asema Mwenyezi Mungu. Ulitumia maneno, ‘Huu ndio ujumbe wa Mwenyezi Mungu,’ Ingawa nilikuambia kuwa kamwe usiseme, ‘Huu ni ujumbe wa Mwenyezi Mungu.’
39Kwa hiyo, hakika nitakusahau na kukutenga mbali na uso wangu pamoja na mji niliowapa ninyi na baba zenu.
40Nitaleta juu yako fedheha ya kudumu: yaani aibu ya kudumu ambayo haitasahaulika.”
Who We AreWhat We EelieveWhat We Do
2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.