Hesabu 8 - Kiswahili Contemporary Scriptures 2024

Kuwekwa kwa taa

1Mwenyezi Mungu akamwambia Musa,

2“Sema na Haruni umwambie, ‘Utakapoziweka zile taa saba, zinatakiwa kuangaza eneo lililo mbele ya kinara cha taa.’ ”

3Haruni akafanya hivyo; akaziweka zile taa ili zielekee mbele kwenye kinara cha taa, kama vile Mwenyezi Mungu alivyomwamuru Musa.

4Hivi ndivyo kinara cha taa kilivyotengenezwa: Kilitengenezwa kwa dhahabu iliyofuliwa, kuanzia kwenye kitako chake hadi kwenye maua yake. Kinara cha taa kilitengenezwa sawasawa kabisa na kielelezo ambacho Mwenyezi Mungu alikuwa amemwonesha Musa.

Kutengwa kwa Walawi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu

5Mwenyezi Mungu akamwambia Musa:

6“Watwae Walawi kutoka miongoni mwa Waisraeli wengine na uwatakase.

7Ili kuwatakasa, fanya hivi: Nyunyizia maji ya utakaso juu yao; kisha uwaambie wanyoe nywele kwenye mwili mzima, wafue nguo zao na hivyo wajitakase wenyewe.

8Waambie wamchukue fahali mchanga pamoja na sadaka yake ya nafaka ya unga laini uliochanganywa na mafuta; kisha utamchukua fahali mchanga wa pili kwa ajili ya sadaka ya dhambi.

9Walete Walawi mbele ya Hema la Kukutania na ukusanye jumuiya yote ya Waisraeli.

10Utawaleta Walawi mbele za Mwenyezi Mungu, na Waisraeli wataweka mikono yao juu ya Walawi.

11Haruni atawaweka Walawi mbele za Mwenyezi Mungu wawe sadaka ya kuinuliwa kutoka kwa Waisraeli, ili wawe tayari kuifanya kazi ya Mwenyezi Mungu.

12“Baada ya Walawi kuweka mikono yao juu ya vichwa vya hao mafahali wawili, tumia mmoja kwa ajili ya sadaka ya dhambi kwa Mwenyezi Mungu, na mwingine kuwa sadaka ya kuteketezwa, ili kufanya upatanisho kwa ajili ya Walawi.

13Waambie hao Walawi wasimame mbele ya Haruni na wanawe, kisha wawatoe wawe sadaka ya kuinuliwa kwa Mwenyezi Mungu.

14Kwa njia hii utakuwa umewatenga Walawi kutoka kwa Waisraeli wengine, nao Walawi watakuwa wangu.

15“Utakapokuwa umekwisha kuwatakasa Walawi na kuwatoa wawe sadaka ya kuinuliwa, watakuja kufanya kazi yao katika Hema la Kukutania.

16Wao ndio Waisraeli ambao watatolewa kabisa kwangu. Nimewatwaa kama mali yangu mwenyewe badala ya mzaliwa wa kwanza, mzaliwa wa kwanza wa kiume kutoka kwa kila mwanamke Mwisraeli.

17Kila mzaliwa wa kwanza wa kiume katika Israeli, awe wa mwanadamu au mnyama, ni wangu. Nilipowaua wazaliwa wote wa kwanza huko Misri, niliwatenga kwa ajili yangu mwenyewe.

18Nami nimewatwaa Walawi badala ya wazaliwa wote wa kwanza wa kiume katika Israeli.

19Kati ya Waisraeli wote, nimempa Haruni na wanawe Walawi kama zawadi ili wafanye kazi katika Hema la Kukutania kwa niaba ya Waisraeli, na kufanya upatanisho kwa ajili yao ili pasiwepo na pigo lolote litakalowapata Waisraeli wakati watakapokaribia mahali patakatifu.”

20Musa, Haruni na jumuiya yote ya Waisraeli wakawafanyia Walawi kama Mwenyezi Mungu alivyomwamuru Musa.

21Walawi wakajitakasa wenyewe na wakafua nguo zao. Kisha Haruni akawasogeza mbele za Mwenyezi Mungu kuwa sadaka ya kuinuliwa, na kufanya upatanisho kwa ajili yao ili kuwatakasa.

22Baada ya hayo, Walawi walikuja kufanya kazi yao katika Hema la Kukutania chini ya usimamizi wa Haruni na wanawe. Waliwafanyia Walawi kama vile Mwenyezi Mungu alivyomwamuru Musa.

23Mwenyezi Mungu akamwambia Musa,

24“Hili linawahusu Walawi: Wanaume wenye umri wa miaka ishirini na tano au zaidi watakuja kushiriki katika kazi kwenye Hema la Kukutania,

25lakini watakapofika umri wa miaka hamsini, ni lazima waache kazi zao za kawaida wala wasiendelee.

26Wanaweza kuwasaidia ndugu zao kufanya wajibu wao katika Hema la Kukutania, lakini wao wenyewe kamwe hawatafanya hiyo kazi. Basi, hivi ndivyo utakavyogawa wajibu kwa Walawi.”

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help