Ayubu 16 - Kiswahili Contemporary Scriptures 2024

Hotuba ya tano ya AyubuAyubu anajibu: Hakika sina hatia

1Kisha Ayubu akajibu:

2“Nimepata kusikia mambo mengi kama haya,

nanyi nyote ni wafariji wenye kutaabisha!

3Je, maneno yenu mengi yasiyo na maana hayana mwisho?

Mna nini hata mwendelee kushindana kwa maneno?

4Mimi pia ningeweza kuzungumza kama ninyi,

kama mngekuwa katika hali yangu;

ningeweza kutoa hotuba nzuri dhidi yenu,

na kuwatikisia ninyi kichwa changu.

5Lakini kinywa changu kingewatia moyo;

faraja kutoka mdomoni mwangu ingewaletea nafuu.

6“Lakini nikisema, maumivu yangu bado hayatulizwi;

na nikijizuia, bado hayaondoki.

7Ee Mungu, hakika umenichakaza;

umewaangamiza kabisa watu wa nyumbani mwangu wote.

8Umenikunjakunja, nalo limekuwa ushahidi;

nako kukonda kwangu kumeongezeka sana na kushuhudia dhidi yangu.

9Mungu amenishambulia na kunirarua katika hasira yake,

na kunisagia meno yake;

adui yangu hunikazia macho yake makali.

10Watu wamenifumbulia vinywa vyao kunidhihaki;

hunipiga shavuni mwangu kwa dharau,

na kuungana pamoja dhidi yangu.

11Mungu amenigeuzia kwa watu wapotovu,

na kunitupa katika makucha ya waovu.

12Mambo yote yalikuwa mazuri, lakini alinivunjavunja;

amenikamata shingo na kuniponda.

Amenifanya mimi kuwa shabaha yake;

13wapiga upinde wake wananizunguka.

Bila huruma, huchoma figo zangu,

na kuimwaga nyongo yangu juu ya nchi.

14Huniponda tena na tena;

hunishambulia kama shujaa wa vita.

15“Nimejishonea gunia juu ya mwili wangu,

nami nimezika paji la uso wangu kwenye vumbi.

16Uso wangu umekuwa mwekundu kwa kulia,

macho yangu yamepigwa na giza.

17Hata hivyo mikono yangu haijafanya jeuri,

na maombi yangu ni safi.

18“Ee nchi, usiifunike damu yangu,

nacho kilio changu kisinyamazishwe kamwe.

19Hata sasa shahidi wangu yuko mbinguni;

wakili wangu yuko juu.

20Mwombezi wangu ni rafiki yangu

macho yangu yanapomwaga machozi kwa Mungu;

21kwa niaba ya mtu anamsihi Mungu

kama mtu anavyosihi kwa ajili ya rafiki yake.

22“Ni miaka michache tu itapita

kabla sijaenda safari ambayo sitarudi.

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help