1 Wafalme 9 - Kiswahili Contemporary Scriptures 2024

Mwenyezi Mungu amtokea Sulemani(2 Nyakati 7:11-22)

1Sulemani alipomaliza kujenga Hekalu la Mwenyezi Mungu na jumba la kifalme, na alipokwisha kufanya yote aliyotaka kufanya,

2Mwenyezi Mungu akamtokea mara ya pili, vile alivyomtokea huko Gibeoni.

3Mwenyezi Mungu akamwambia:

“Nimesikia dua na maombi uliyofanya mbele zangu, nimeliweka wakfu Hekalu hili ambalo umelijenga, kwa kuweka Jina langu humo milele. Macho yangu na moyo wangu utakuwa humo siku zote.

4“Kwako wewe, kama ukienenda kwa unyofu wa moyo na uadilifu, kama baba yako Daudi alivyofanya na kutenda yote ninayoyaagiza kwa kutunza maagizo yangu na sheria,

5nitakiimarisha kiti chako cha utawala juu ya Israeli milele kama nilivyomwahidi Daudi baba yako niliposema, ‘Hutakosa kamwe kuwa na mtu kwenye kiti cha utawala cha Israeli.’

6“Lakini ninyi au wana wenu mkinigeukia mbali na kuziacha amri na maagizo yangu niliyowapa na kwenda kuitumikia miungu mingine na kuiabudu,

7basi nitakatilia mbali Israeli kutoka nchi niliyowapa, nami nitalikataa Hekalu hili nililolitakasa kwa ajili ya Jina langu. Ndipo Israeli itakuwa kitu cha kudharauliwa na watu na kuwa kitu cha kudhihakiwa miongoni mwa watu wote.

8Ingawa hekalu hili linavutia sasa, wote watakaolipita watashangaa na kudhihaki wakisema, ‘Kwa nini Mwenyezi Mungu amefanya kitu kama hiki katika nchi hii na kwa Hekalu hili?’

9Watu watajibu, ‘Kwa sababu wamemwacha Mwenyezi Mungu, Mungu wao, aliyewatoa baba zao Misri, nao wamekumbatia miungu mingine, wakaiabudu na kuitumikia, ndiyo sababu Mwenyezi Mungu ameyaleta maafa haya yote juu yao.’ ”

Shughuli nyingine za Sulemani(2 Nyakati 8)

10Miaka ishirini ilipopita, muda ambao Sulemani alijenga majengo haya mawili, yaani Hekalu la Mwenyezi Mungu na jumba la kifalme,

11Mfalme Sulemani akampa Hiramu mfalme wa Tiro miji ishirini katika Galilaya, kwa sababu Hiramu alikuwa amempatia mierezi na misunobari yote na dhahabu yote kama alivyohitaji.

12Lakini Hiramu alipotoka Tiro kwenda kuiona ile miji ambayo Sulemani alikuwa amempa, hakupendezwa nayo.

13Hiramu akauliza, “Hii ni miji ya namna gani uliyonipa, ndugu yangu?”

Naye akaiita nchi ya Kabul, jina lililoko hadi leo.

14Basi Hiramu alikuwa amempelekea mfalme talanta mia moja na ishirini za dhahabu.

15Haya ni maelezo kuhusu kazi za kulazimishwa ambazo Mfalme Sulemani aliwafanyiza watu ili kulijenga Hekalu la Mwenyezi Mungu, na jumba lake la kifalme, na Milo, ukuta wa Yerusalemu, Hazori, Megido na Gezeri.

16(Farao mfalme wa Misri alikuwa ameushambulia na kuuteka mji wa Gezeri. Alikuwa ameuchoma moto. Akawaua Wakanaani waliokuwa wakikaa humo na kisha kuutoa kwa binti yake, yaani mkewe Sulemani, kama zawadi ya arusi.

17Sulemani akaujenga tena Gezeri.) Akajenga Beth-Horoni ya Chini,

18akajenga Baalathi na Tamari kwenye jangwa katika eneo la nchi yake.

19Vilevile, alijenga miji ya ghala na ya magari yake ya vita na kwa ajili ya farasi wake na wapanda farasi: alijenga kila alichotaka katika Yerusalemu, katika Lebanoni, na katika eneo lote alilotawala.

20Watu wote waliosalia miongoni mwa Waamori, Wahiti, Waperizi, Wahivi, na Wayebusi (watu wasiokuwa Waisraeli),

21yaani, wazao wao waliobakia katika nchi, ambao Waisraeli hawakuwaangamiza kabisa, Sulemani akawalazimisha kuwa shokoa, kama ilivyo hadi leo.

22Lakini Sulemani hakumfanya Mwisraeli yeyote kuwa mtumwa; hao ndio walikuwa wapiganaji wake, viongozi wa serikali yake, maafisa wake, wakuu wake wa jeshi, majemadari wa magari yake ya vita, na wapanda farasi wake.

23Pia walikuwa maafisa wakuu wasimamizi wa miradi ya Sulemani: maafisa mia tano na hamsini waliwasimamia watu waliofanya kazi.

24Baada ya binti Farao kuja kutoka Mji wa Daudi na kuingia jumba la kifalme ambalo Sulemani alikuwa amemjengea, Sulemani akajenga Milo.

25Sulemani akatoa dhabihu za kuteketezwa na sadaka za amani mara tatu kwa mwaka juu ya madhabahu aliyokuwa amemjengea Mwenyezi Mungu. Pamoja na hizo dhabihu, akafukiza uvumba mbele za Mwenyezi Mungu, hivyo kutimiza kanuni za Hekalu.

26Mfalme Sulemani pia akatengeneza meli huko Esion-Geberi, iliyo karibu na Elathi katika Edomu, kwenye ukingo wa Bahari ya Shamu.

27Naye Hiramu akawatuma watu wake; mabaharia walioijua bahari, kuhudumu katika hizo meli pamoja na watu wa Sulemani.

28Wakasafiri kwa bahari hadi Ofiri na kurudi na talanta mia nne na ishirini (420) za dhahabu, ambazo walimkabidhi Mfalme Sulemani.

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help