Yeremia 6 - Kiswahili Contemporary Scriptures 2024

Yerusalemu kuzingirwa na jeshi

1“Kimbieni kwa usalama wenu, enyi watu wa Benyamini!

Kimbieni kutoka Yerusalemu!

Pigeni tarumbeta katika Tekoa!

Inueni ishara juu ya Beth-Hakeremu!

Kwa kuwa maafa yanaonekana yakitoka kaskazini,

na uharibifu wa kutisha.

2Nitamwangamiza Binti Sayuni,

aliye mzuri sana na mwororo.

3Wachungaji pamoja na makundi yao

watakuja dhidi yake;

watapiga mahema yao kumzunguka,

kila mmoja akichunga kundi lake mwenyewe.”

4“Jiandaeni kwa vita dhidi yake!

Inukeni tumshambulie mchana!

Lakini, ole wetu, mchana unaisha,

na vivuli vya jioni vinazidi kuwa virefu.

5Kwa hiyo inukeni, tufanye mashambulizi usiku,

na kuharibu ngome zake!”

6Hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni:

“Kateni miti mjenge boma

kuzingira Yerusalemu.

Mji huu ni lazima uadhibiwe;

umejazwa na uonevu.

7Kama vile kisima kinavyomwaga maji yake,

ndivyo anavyomwaga uovu wake.

Ukatili na maangamizi vyasikika ndani yake,

ugonjwa wake na majeraha yake viko mbele yangu daima.

8Pokea onyo, ee Yerusalemu,

la sivyo nitageukia mbali nawe

na kuifanya nchi yako kuwa ukiwa,

asiweze mtu kuishi ndani yake.”

9Hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni:

“Wao na wayakusanye mabaki ya Israeli

kwa uangalifu kama kwenye mzabibu;

pitisha mkono wako kwenye matawi tena,

kama yeye avunaye zabibu.”

10Niseme na nani na kumpa onyo?

Ni nani atakayenisikiliza mimi?

Masikio yao yameziba,

kwa hiyo hawawezi kusikia.

Neno la Mwenyezi Mungu ni chukizo kwao,

hawalifurahii.

11Lakini nimejaa ghadhabu ya Mwenyezi Mungu,

nami siwezi kuizuia.

“Wamwagie watoto walio barabarani,

na juu ya vijana wa kiume waliokusanyika;

mume na mke watakumbwa pamoja ndani yake,

hata nao wazee waliolemewa na miaka.

12Nyumba zao zitapewa watu wengine,

pamoja na mashamba yao na wake zao,

nitakapounyoosha mkono wangu

dhidi ya wale wanaoishi katika nchi,”

asema Mwenyezi Mungu.

13“Kuanzia aliye mdogo kabisa hadi aliye mkubwa kabisa,

wote wana tamaa ya kupata faida zaidi;

manabii na makuhani wanafanana,

wote wanafanya udanganyifu.

14Wanafunga majeraha ya watu wangu

bila uangalifu.

Wanasema, ‘Amani, amani,’

wakati hakuna amani.

15Je, wanaona aibu kwa ajili ya tabia yao

inayochukiza mno?

Hapana, hawana haya hata kidogo;

hawajui hata kuona aibu.

Kwa hiyo wataanguka miongoni mwa hao walioanguka,

watashushwa chini nitakapowaadhibu,”

asema Mwenyezi Mungu.

16Hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu:

“Simama kwenye njia panda utazame,

ulizia mapito ya zamani,

ulizia wapi ilipo njia nzuri, uifuate hiyo,

nanyi mtapata amani nafsini mwenu.

Lakini ninyi mlisema, ‘Hatutaipita njia hiyo.’

17Niliweka walinzi juu yenu na kusema,

‘Sikieni sauti ya tarumbeta!’

Lakini mkasema, ‘Hatutasikiliza.’

18Kwa hiyo sikilizeni, enyi mataifa,

angalieni, enyi mashahidi,

lile litakalowatokea.

19Sikia, ee nchi:

Ninaleta maafa juu ya watu hawa,

matunda ya mipango yao,

kwa sababu hawakusikiliza maneno yangu

na wameikataa sheria yangu.

20Unanifaa nini uvumba kutoka Sheba,

au udi wa harufu nzuri kutoka nchi ya mbali?

Sadaka zako za kuteketezwa hazikubaliki,

dhabihu zako hazinifurahishi mimi.”

21Kwa hiyo hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu:

“Nitaweka vikwazo mbele ya watu hawa.

Baba na wana wao watajikwaa juu yake,

majirani na rafiki wataangamia.”

22Hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu:

“Tazama, jeshi linakuja

kutoka nchi ya kaskazini,

taifa kubwa linaamshwa

kutoka miisho ya dunia.

23Wamejifunga pinde na mkuki,

ni wakatili na hawana huruma.

Wanatoa sauti kama bahari inayounguruma

wanapoendesha farasi wao.

Wanakuja kama watu waliojipanga tayari kwa vita

ili kukushambulia, ee Binti Sayuni.”

24Tumesikia taarifa zao,

nayo mikono yetu imelegea.

Uchungu umetushika,

maumivu kama ya mwanamke katika uchungu wa kuzaa.

25Usitoke kwenda mashambani

au kutembea barabarani,

kwa kuwa adui ana upanga,

na kuna vitisho kila upande.

26Enyi watu wangu, vaeni magunia

mjivingirishe kwenye majivu,

ombolezeni kwa kilio cha uchungu

kama amliliaye mwana pekee,

kwa maana ghafula

mharibu atatujia.

27“Nimekufanya wewe kuwa kitu cha kujaribu chuma,

nao watu wangu kama mawe yenye madini,

ili upate kuzijua na kuzijaribu njia zao.

28Wote ni waasi sugu,

wakienda huku na huko kusengenya.

Wao ni shaba na chuma,

wote wanatenda upotovu.

29Mivuo inavuma kwa nguvu,

kinachoungua kwa huo moto ni risasi,

lakini pamoja na kusafisha kote huku ni bure;

waovu hawaondolewi.

30Wanaitwa fedha iliyokataliwa,

kwa sababu Mwenyezi Mungu amewakataa.”

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help