1Nitakutukuza wewe, Ee Mwenyezi Mungu,
kwa kuwa umeniinua kutoka vilindi,
na hukuacha adui zangu
washangilie juu yangu.
2Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wangu, nilikuita unisaidie
na wewe umeniponya.
3Ee Mwenyezi Mungu, umenitoa Kuzimu,
umeniokoa nisishuke kwenye shimo la mauti.
4Mwimbieni Mwenyezi Mungu, enyi watakatifu wake;
lisifuni jina lake takatifu.
5Kwa maana hasira yake ni ya muda mfupi,
bali upendo wake hudumu siku zote.
Inawezekana kilio kiwepo usiku kucha,
lakini furaha huja asubuhi.
6Nilipofanikiwa nilisema,
“Sitatikiswa kamwe.”
7Ee Mwenyezi Mungu, uliponijalia,
uliuimarisha mlima wangu,
lakini ulipouficha uso wako
nilifadhaika.
8Kwako wewe, Ee Mwenyezi Mungu, niliita,
niliomba rehema kwa Bwana:
9“Kuna faida gani katika kuangamia kwangu,
katika kushuka kwangu shimoni?
Je, mavumbi yatakusifu?
Je, yatatangaza uaminifu wako?
10Ee Mwenyezi Mungu, unisikie na kunihurumia;
Ee Mwenyezi Mungu, uwe msaada wangu.”
11Uligeuza maombolezo yangu kuwa kucheza,
ulinivua gunia ukanivika shangwe,
12ili moyo wangu uweze kukusifu na usikae kimya.
Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wangu, nitakushukuru milele.
Who We AreWhat We EelieveWhat We Do
2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.