Yeremia 12 - Kiswahili Contemporary Scriptures 2024

Lalamiko la Yeremia

1Wewe daima u mwenye haki, Ee Mwenyezi Mungu,

niletapo mashtaka mbele yako.

Hata hivyo nitazungumza nawe kuhusu hukumu yako:

Kwa nini njia ya waovu inafanikiwa?

Kwa nini wasio waaminifu

wote wanaishi salama?

2Umewapanda, nao wameota,

wanakua na kuzaa matunda.

Daima u midomoni mwao,

lakini mbali na mioyo yao.

3Hata hivyo unanijua mimi, Ee Mwenyezi Mungu;

unaniona na kuyachunguza mawazo yangu kukuhusu wewe.

Wakokote kama kondoo wanaoenda kuchinjwa!

Watenge kwa ajili ya siku ya kuchinjwa!

4Je, nchi itakaa katika hali ya kuomboleza hadi lini,

na majani katika kila shamba kunyauka?

Kwa sababu wale wanaoishi ndani yake ni waovu,

wanyama na ndege wameangamia.

Zaidi ya hayo, watu wanasema,

“Mwenyezi Mungu hataona yatakayotupata sisi.”

Jibu la Mwenyezi Mungu

5“Ikiwa umeshindana mbio na watu kwa mguu na wakakushinda,

unawezaje kushindana na farasi?

Ikiwa unajikwaa kwenye nchi ambayo ni salama,

utawezaje kwenye vichaka kando ya Yordani?

6Ndugu zako na jamaa zako nao wamekusaliti,

wameinua kilio kikubwa dhidi yako.

Usiwaamini hata wakisema

mema juu yako.

7“Nitaiacha nyumba yangu,

nitupe urithi wangu;

nitamtia yeye nimpendaye

mikononi mwa adui zake.

8Urithi wangu umekuwa kwangu

kama simba wa msituni.

Nauchukia kwa kuwa

unaningurumia.

9Je, urithi wangu haukuwa

kama ndege wa mawindo wa madoadoa

ambaye ndege wengine wawindao

humzunguka na kumshambulia?

Nenda ukawakusanye pamoja wanyama wote wa mwituni;

walete ili wale.

10Wachungaji wengi wataliharibu shamba langu la mizabibu

na kulikanyaga shamba langu;

watalifanya shamba langu zuri

kuwa jangwa la ukiwa.

11Litafanywa kuwa jangwa,

lililokauka na kuachwa ukiwa mbele zangu;

nchi yote itafanywa jangwa

kwa sababu hakuna hata mmoja anayejali.

12Juu ya miinuko yote ilivyo kama jangwani

waangamizi watavamia,

kwa maana upanga wa Mwenyezi Mungu utawala,

kuanzia ncha moja ya nchi hadi nyingine;

hakuna hata mmoja atakayekuwa salama.

13Watapanda ngano lakini watavuna miiba;

watajitaabisha lakini hawatafaidi chochote.

Kwa hiyo beba aibu ya mavuno yako

kwa sababu ya hasira kali ya Mwenyezi Mungu.”

14Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: “Kwa habari ya majirani zangu wote wabaya wanaonyang’anya urithi ambao ninawapa watu wangu Israeli, nitawang’oa kutoka nchi zao, nami nitaing’oa nyumba ya Yuda kutoka katikati yao.

15Lakini baada ya kuwang’oa, nitawahurumia tena na kumrudisha kila mmoja wao kwenye urithi wake mwenyewe na kwenye nchi yake mwenyewe.

16Ikiwa watajifunza vyema njia za watu wangu na kuapa kwa Jina langu, wakisema, ‘Hakika kama Mwenyezi Mungu aishivyo,’ hata kama wakati fulani walifundisha watu wangu kuapa kwa Baali, ndipo watafanywa imara katikati ya watu wangu.

17Lakini kama taifa lolote halitasikiliza na kutii, nitaling’oa kabisa na kuliangamiza,” asema Mwenyezi Mungu.

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help