Zaburi 77 - Kiswahili Contemporary Scriptures 2024

Zaburi 77Matendo makuu ya Mwenyezi Mungu yanakumbukwaKwa mwimbishaji. Mtindo wa Yeduthuni. Zaburi ya Asafu.

1Nilimlilia Mungu ili anisaidie,

nilimlilia Mungu ili anisikie.

2Nilipokuwa katika taabu, nilimtafuta Bwana,

usiku nilinyoosha mikono bila kuchoka

na nafsi yangu ilikataa kufarijika.

3Ee Mungu, nilikukumbuka wewe, nikalia kwa huzuni;

nikatafakari, roho yangu ikadhoofika.

4Ulizuia macho yangu kufumba;

nilikuwa nasumbuka, nikashindwa kusema.

5Nilitafakari kuhusu siku zilizopita,

miaka mingi iliyopita,

6nilikumbuka nilivyoimba nyimbo usiku.

Moyo wangu ulitafakari

na roho yangu ikauliza:

7“Je, Bwana atakataa milele?

Je, hatatenda mema tena?

8Je, upendo wake usio na mwisho umetoweka milele?

Je, ahadi yake imekoma nyakati zote?

9Je, Mungu amesahau kuwa na huruma?

Je, katika hasira amezuia fadhili zake?”

10Ndipo nikawaza, “Huu ndio udhaifu wangu:

lakini nitakumbuka

miaka ya mkono wa kuume

wa Aliye Juu Sana.”

11Nitayakumbuka matendo ya Mwenyezi Mungu;

naam, nitaikumbuka miujiza yako ya zamani.

12Nitazitafakari kazi zako zote

na kuyawaza matendo yako makuu.

13Ee Mungu, njia zako ni takatifu.

Ni mungu yupi aliye mkuu kama Mungu wetu?

14Wewe ndiwe Mungu utendaye miujiza,

umeonesha uwezo wako kati ya mataifa.

15Kwa mkono wako wenye nguvu umewakomboa watu wako,

uzao wa Yakobo na Yusufu.

16Maji yalikuona, Ee Mungu,

maji yalikuona yakakimbia,

vilindi vilitetemeka.

17Mawingu yalimwaga maji,

mbingu zikatoa ngurumo kwa radi;

mishale yako ilimetameta huku na huko.

18Ngurumo yako ilisikika katika upepo wa kisulisuli,

umeme wako wa radi ukaangaza dunia,

nchi ikatetemeka na kutikisika.

19Njia yako ilipita baharini,

mapito yako kwenye maji makuu,

ingawa nyayo zako hazikuonekana.

20Uliongoza watu wako kama kundi

kwa mkono wa Musa na Haruni.

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help