Zekaria 6 - Kiswahili Contemporary Scriptures 2024

Maono ya nane: Magari manne ya vita

1Nikatazama juu tena: nikaona mbele yangu magari manne ya vita yakija kutoka kati ya milima miwili, milima ya shaba!

2Gari la kwanza lilivutwa na farasi wekundu, la pili lilivutwa na farasi weusi,

3la tatu lilivutwa na farasi weupe, na gari la nne lilivutwa na farasi wa madoadoa ya kijivu, wote wenye nguvu.

4Nikamuuliza malaika aliyekuwa akizungumza nami, “Hawa ni nani, bwana wangu?”

5Malaika akanijibu, “Hizi ni roho nne za mbinguni zisimamazo mbele ya uwepo wa Bwana wa dunia yote, zinatoka kwenda kufanya kazi yake.

6Gari linalovutwa na farasi weusi linaelekea katika nchi ya kaskazini, la farasi weupe linaelekea magharibi, na la farasi wa madoadoa ya kijivu linaelekea kusini.”

7Hao farasi wenye nguvu walipokuwa wakitoka, walikuwa wakijitahidi kwenda duniani kote. Akasema, “Nenda duniani kote!” Kwa hiyo wakaenda duniani kote.

8Kisha akaniita, “Tazama, wale wanaoenda kuelekea nchi ya kaskazini wamepumzisha Roho wangu Mtakatifu katika nchi ya kaskazini.”

Taji kwa ajili ya Yoshua

9Neno la Mwenyezi Mungu likanijia kusema:

10“Chukua fedha na dhahabu kutoka kwa watu waliohamishwa, yaani Heldai, Tobia na Yedaya ambao wamefika kutoka Babeli. Siku hiyo hiyo nenda nyumbani mwa Yosia mwana wa Sefania.

11Chukua fedha na dhahabu utengeneze taji, nawe uliweke kichwani mwa kuhani mkuu Yoshua, mwana wa Yehosadaki.

12Umwambie hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni: ‘Huyu ndiye mtu anayeitwa Tawi, naye atachipua kutoka mahali pake na kujenga Hekalu la Mwenyezi Mungu.

13Ni yeye atakayejenga Hekalu la Mwenyezi Mungu, naye atavikwa utukufu na ataketi kumiliki kwenye kiti cha enzi. Atakuwa kuhani kwenye kiti chake cha enzi. Hapo patakuwa na amani kati ya hao wawili.’

14Taji litatolewa kwa Heldai, Tobia, Yedaya na Heni mwana wa Sefania kama kumbukumbu ndani ya Hekalu la Mwenyezi Mungu.

15Wale walio mbali sana watakuja na kusaidia kulijenga Hekalu la Mwenyezi Mungu, nanyi mtajua kuwa Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni amenituma kwenu. Hili litatokea ikiwa mtamtii Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, kwa bidii.”

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help