1Baada ya Yekonia mwana wa Yehoyakimu mfalme wa Yuda, pamoja na maafisa, mafundi stadi na wahunzi wa Yuda, kuchukuliwa kutoka Yerusalemu kwenda uhamishoni Babeli na Nebukadneza, mfalme wa Babeli, Mwenyezi Mungu akanionesha vikapu viwili vya tini vilivyowekwa mbele ya Hekalu la Mwenyezi Mungu.
2Kikapu kimoja kilikuwa na tini nzuri sana, kama zile za mavuno ya kwanza. Kikapu cha pili kilikuwa na tini dhaifu sana, mbovu mno zisizofaa kuliwa.
3Kisha Mwenyezi Mungu akaniuliza, “Je, Yeremia, unaona nini?”
Nikamjibu, “Ninaona tini zilizo nzuri ni nzuri sana, lakini zilizo mbaya, ni mbaya sana zisizofaa kuliwa.”
4Kisha neno la Mwenyezi Mungu likanijia:
5“Hili ndilo Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, asemalo: ‘Kama zilivyo hizi tini nzuri, ndivyo ninavyowaona kuwa bora watu wa uhamisho kutoka Yuda, niliowaondoa kutoka mahali hapa kwenda katika nchi ya Wakaldayo.
6Macho yangu yatakuwa juu yao kwa ajili ya kuwapatia mema, nami nitawarudisha tena katika nchi hii. Nitawajenga wala sitawabomoa, nitawapanda wala sitawang’oa,
7nitawapa moyo wa kunifahamu mimi, kwamba mimi ndimi Mwenyezi Mungu. Watakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wao, kwa maana watanirudia kwa moyo wote.
8“ ‘Lakini kama zilivyo zile tini dhaifu, ambazo ni mbovu mno zisizofaa kuliwa,’ asema Mwenyezi Mungu, ‘ndivyo nitakavyomtendea Sedekia mfalme wa Yuda, maafisa wake, na mabaki wengine kutoka Yerusalemu, wawe wamebaki katika nchi hii, au wanaishi Misri.
9Nitawafanya kuwa chukizo kabisa na kitu cha kulaumiwa katika mataifa yote ya dunia, watakuwa aibu na kitu cha kudharauliwa, chombo cha dhihaka na kulaaniwa, popote nitakapowafukuzia.
10Nitautuma upanga, njaa na tauni dhidi yao hadi wawe wameangamia kutoka nchi niliyowapa wao na baba zao.’ ”
Who We AreWhat We EelieveWhat We Do
2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.