2 Wafalme 2 - Kiswahili Contemporary Scriptures 2024

Ilya achukuliwa mbinguni

1Mwenyezi Mungu alipokuwa karibu kumchukua Ilya mbinguni kwa upepo wa kisulisuli, Ilya na Al-Yasa walikuwa njiani wakitoka Gilgali.

2Ilya akamwambia Al-Yasa, “Kaa hapa. Mwenyezi Mungu amenituma Betheli.”

Lakini Al-Yasa akasema, “Hakika kama Mwenyezi Mungu aishivyo na wewe uishivyo, sitakuacha.” Kwa hiyo wakaenda Betheli pamoja.

3Wana wa manabii waliokuwa Betheli wakamjia Al-Yasa na kumuuliza, “Je, unajua kwamba Mwenyezi Mungu atakuondolea bwana wako leo?”

Al-Yasa akawajibu, “Ndiyo, najua, lakini msizungumze kuhusu jambo hilo.”

4Kisha Ilya akamwambia, “Baki hapa, Al-Yasa. Mwenyezi Mungu amenituma Yeriko.”

Naye akajibu, “Kwa hakika kama Mwenyezi Mungu aishivyo na wewe uishivyo, sitakuacha.” Hivyo wakaenda Yeriko.

5Wana wa manabii waliokuwa Yeriko wakamwendea Al-Yasa na kumuuliza, “Je, unajua kwamba Mwenyezi Mungu atakuondolea bwana wako leo?”

Akawajibu, “Ndiyo, najua, lakini msizungumze juu ya jambo hilo.”

6Kisha Ilya akamwambia, “Kaa hapa. Mwenyezi Mungu amenituma kwenda Yordani.”

Naye akamjibu, “Kwa hakika kama Mwenyezi Mungu aishivyo na wewe uishivyo, sitakuacha.” Hivyo wote wawili wakaendelea pamoja.

7Wana hamsini wa manabii wakaenda na kusimama kwa mbali, kuelekea mahali Ilya na Al-Yasa waliposimama kando ya Mto Yordani.

8Ilya akatoa vazi lake, akalikunja na kupiga maji nalo. Maji yakagawanyika upande wa kuume na upande wa kushoto, nao wawili wakavuka pakavu.

9Walipokwisha kuvuka, Ilya akamwambia Al-Yasa, “Niambie, nikufanyie nini kabla sijaondolewa kutoka kwako?”

Al-Yasa akajibu, “Naomba nirithi sehemu maradufu ya roho yako.”

10Ilya akasema, “Umeomba jambo gumu. Lakini kama utaniona wakati ninapoondolewa kutoka kwako litakuwa lako. La sivyo, hutalipata.”

11Walipokuwa wakitembea pamoja na kuzungumza, ghafula gari la farasi la moto na farasi wa moto vilitokea na kuwatenganisha wao wawili, naye Ilya akapanda mbinguni katika upepo wa kisulisuli.

12Al-Yasa aliliona hili, naye akapaza sauti, “Baba yangu! Baba yangu! Magari ya vita ya Israeli na wapanda farasi wake!” Naye Al-Yasa hakumwona tena. Kisha akaishika nguo yake na kuirarua vipande viwili.

13Akaliokota lile vazi lililoanguka kutoka kwa Ilya, kisha akarudi na kusimama ukingoni mwa Yordani.

14Ndipo akalichukua lile vazi ambalo lilikuwa limeanguka kutoka kwa Ilya, naye akayapiga yale maji nalo. Akauliza, “Yuko wapi sasa Mwenyezi Mungu, Mungu wa Ilya?” Al-Yasa alipoyapiga maji, yakagawanyika kulia na kushoto, naye akavuka.

15Wale wana wa manabii kutoka Yeriko waliokuwa wakitazama wakasema, “Roho ya Ilya inamkalia Al-Yasa.” Nao wakaenda kumlaki na kusujudu hadi chini mbele yake.

16Wakasema, “Tazama, sisi watumishi wako tunao watu hamsini wenye uwezo. Waruhusu waende kumtafuta bwana wako. Labda Roho wa Mwenyezi Mungu amemtwaa na kumweka katika mlima fulani au bonde fulani.”

Al-Yasa akajibu, “Hapana, msiwatume.”

17Lakini wakasisitiza, hata akaona aibu kuwakatalia. Hivyo akasema, “Watumeni.” Nao wakawatuma watu hamsini, wakamtafuta kwa siku tatu, lakini hawakumpata.

18Walipomrudia Al-Yasa, aliyekuwa akingojea huko Yeriko, akawaambia, “Je, sikuwaambia msiende?”

Kuponywa kwa maji

19Watu wa mji wakamwambia Al-Yasa, “Tazama, bwana wetu, mahali mji huu ulipojengwa ni pazuri, kama bwana wangu anavyoona, lakini maji yake ni mabaya, na nchi haina mazao.”

20Akasema, “Nileteeni bakuli mpya, mweke chumvi ndani yake.” Kwa hiyo wakamletea.

21Kisha akaenda kwenye chemchemi na kuitupa ile chumvi ndani yake, akisema, “Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: ‘Nimeyaponya maji haya. Kamwe hayatasababisha mauti tena wala kutozaa.’ ”

22Nayo yale maji yakaponywa hadi leo, sawasawa na neno la Al-Yasa alilokuwa amesema.

Al-Yasa afanyiwa mzaha

23Kutoka huko Al-Yasa akakwea kwenda Betheli. Ikawa alipokuwa akitembea barabarani, baadhi ya vijana wakatoka mjini na kumfanyia mzaha. Wakasema, “Paa, wewe mwenye upara! Paa, wewe mwenye upara!”

24Akageuka, akawatazama na kuwalaani kwa Jina la Mwenyezi Mungu. Kisha dubu jike wawili wakatokea mwituni na kuwararua vijana arobaini na wawili miongoni mwao.

25Naye akaondoka huko, akaenda Mlima Karmeli, na kutoka huko akarudi Samaria.

Blog
About Us
Message
Site Map

Who We AreWhat We EelieveWhat We Do

Terms of UsePrivacy Notice

2025 by iamachristian.org,Inc All rights reserved.

Home
Gospel
Question
Blog
Help